Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Judith Kapinga, amesema Serikali imeendelea kuweka mkazo mkubwa katika maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na kuwawezesha wajasiriamali nchini.
Waziri huyo ameyasema hayo leo Mei 22, wakati akiwasilisha bungeni bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.Katika hotuba yake, Waziri huyo amesema Serikali imepanga kuanzisha na kuendeleza miundombinu ya viwanda, kufanya tafiti kwenye sekta za vipaumbele pamoja na kukamilisha kanzidata ya viwanda nchini ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo. Ameeleza kuwa hatua hizo zimekusudia kuongeza mchango wa viwanda katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Aidha, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limeendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma, chuma cha Liganga pamoja na mradi wa Magadi Soda Engaruka. Serikali pia imeendelea kuboresha Kiwanda cha Mashine na Vipuri cha KMTC pamoja na kufufua Kiwanda cha Mang’ula kwa kushirikiana na wawekezaji.
Katika hatua nyingine, Serikali imeendelea kuimarisha kongani za viwanda kwa kuboresha miundombinu yake na kuanzisha kongani kubwa za kisasa zitakazovutia wawekezaji zaidi. Sambamba na hilo, mashamba ya miti ya mpira yanaendelezwa kwa ajili ya kuzalisha malighafi za viwanda huku yakichangia uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Serikali imepanga kuanzisha Kituo cha Taarifa za Viwanda (NIIMS) pamoja na kufanya tafiti kuhusu madini adimu katika mikoa ya Kagera, Singida na Dodoma. Pia maabara mbalimbali zimeendelea kuboreshwa ili kuongeza uwezo wa upimaji na ubora wa bidhaa za viwandani.
TIRDO pia imepanga kujenga kiwanda darasa cha vifaa vya kielektroniki vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini pamoja na mtambo wa kisasa wa biogas jijini Dar es Salaam utakaobadilisha taka kuwa gesi ya LPG katika masoko ya Mabibo, Ilala Boma na Temeke Stereo.
Wakati huo huo, taasisi za CAMARTEC, SIDO na TEMDO zimeendelea kuweka mikakati ya kuwawezesha wajasiriamali nchini kwa kutoa mafunzo, mikopo na kuwatafutia masoko. Serikali imepanga kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 21,200 kupitia programu za ukuzaji ujuzi na teknolojia za uzalishaji.
Katika sekta ya biashara, Wizara imeendelea kuimarisha ushirikiano wa biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine kupitia mikataba ya kikanda na kimataifa ikiwemo AfCFTA, EAC, SADC pamoja na WTO. Serikali imesema hatua hiyo inalenga kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.
Aidha, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kuratibu maonesho, misafara ya biashara na kufanya intelijensia ya masoko ili kuwasaidia wazalishaji wa ndani kupata masoko mapya ndani na nje ya nchi. Serikali imeeleza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo utaongeza ajira, mapato ya wananchi na kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya viwanda na biashara.

Post a Comment