Na Edward Winchislaus
Wizara ya Viwanda na Biashara imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 137.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini.
Akiwasilisha bajeti hiyo leo Mei 22,2026 Bungeni jijini Dodoma, Waziri Kapinga amesema kati ya fedha zinazoombwa, shilingi bilioni 104.1 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku shilingi bilioni 33.6 zikitengwa kwa matumizi ya maendeleo. Aidha, kati ya fedha za matumizi ya kawaida, zaidi ya shilingi bilioni 78 zitatumika kwa mishahara ya watumishi na bilioni 26.07 kwa matumizi mengineyo.
Katika hotuba yake, Waziri Kapinga amesema bajeti hiyo inalenga kuendelea kuimarisha sekta ya viwanda kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati pamoja na kuboresha mazingira ya biashara nchini. Amesema serikali imejipanga kuongeza uwezo wa uzalishaji viwandani kwa kujenga miundombinu ya kongani za viwanda na mitaa maalumu ya viwanda kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati.
Pia amesema wizara itaendelea kuchochea matumizi ya teknolojia za kisasa, ubunifu na mafunzo ya ujuzi ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi. Serikali pia inalenga kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa wazalishaji viwandani pamoja na wafanyabiashara wadogo ili kukuza uchumi wa viwanda.
Katika mwaka wa fedha 2026/2027, wizara hiyo imeweka mkazo katika kuboresha mazingira ya biashara kwa sekta binafsi pamoja na kuendelea kutafuta masoko mapya ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini. Hatua hiyo inalenga kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Waziri Kapinga amesema mpango na bajeti ya wizara hiyo umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa 2026/27 hadi 2030/31 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025.
Aidha, wizara imeeleza kuwa moja ya maeneo muhimu yatakayopewa kipaumbele ni kuanzishwa kwa Vituo vya Ubunifu na Ukuzaji wa Biashara kwa Vijana (Innovation and Business Hubs). Vituo hivyo vinatarajiwa kuwasaidia vijana wenye mawazo bunifu kupata mazingira ya kuendeleza biashara zao na kushindana katika soko la kimataifa.
Kapinga amesema dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia na uchumi wa kidijitali, hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa Tanzania kuwekeza katika ubunifu wa vijana ili waweze kutumia fursa za biashara za kidijitali zinazokua kwa kasi duniani.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, serikali inaamini kuwa uwekezaji katika viwanda, biashara na ubunifu wa vijana utaongeza ajira, kuchochea uzalishaji wa ndani na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara na viwanda katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Post a Comment