Na Edward Winchislaus
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule, ametangaza rasmi kuanza kwa ununuzi wa mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa msimu wa mwaka 2025/2026, akisema mfumo huo ni hatua muhimu ya kuimarisha soko la mazao na kuongeza tija kwa wakulima wa mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 21, 2026 jijini Dodoma, amesema serikali inalenga kuondoa changamoto zinazowakwamisha wakulima kupata masoko yenye uhakika.
Amesema mfumo huo umeanzishwa kwa lengo la kurasimisha biashara ya mazao ya kilimo na kupunguza changamoto mbalimbali ikiwemo hasara baada ya mavuno, ukosefu wa ubora wa mazao, mabadiliko ya mara kwa mara ya bei pamoja na uhaba wa taarifa sahihi za masoko. Ameongeza kuwa mfumo huo pia unasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa mitaji kwa wakulima na wafanyabiashara.
Mhe. Senyamule amesema mfumo wa stakabadhi ghalani una manufaa makubwa kwa uchumi wa taifa kwani unasaidia upatikanaji wa soko la uhakika, kuongeza uwazi wa bei za mazao na kuwawezesha wakulima kupata taarifa muhimu za uzalishaji na biashara.
Aidha amesema mazao yanayohifadhiwa ghalani yanaweza kutumika kama dhamana ya kupata mikopo benki na hivyo kuongeza uwezo wa wakulima kuendesha shughuli zao za uzalishaji.
Ameeleza kuwa mfumo huo pia unachangia kuhakikisha upatikanaji wa mazao kwa ajili ya viwanda vya usindikaji mwaka mzima, kuongeza mapato ya serikali, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuimarisha usalama wa chakula nchini. Pia amesema mfumo huo unasaidia kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni kupitia mauzo ya mazao nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, Dodoma ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya ufuta, mbaazi na dengu ambayo huuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. Amesema utekelezaji wa mfumo huo ulianza mwaka 2024 na mwaka 2025 wakulima wa mkoa huo waliuza zaidi ya kilogramu bilioni 46 za mazao na kupata zaidi ya shilingi bilioni 82 kupitia mauzo hayo.
Katika maandalizi ya msimu wa mwaka huu, amesema mkoa umeendelea kutoa elimu kwa wadau wa mfumo huo pamoja na kuongeza maghala ya kukusanyia mazao ambapo jumla ya maghala 39 yameandaliwa katika halmashauri mbalimbali zikiwemo Bahi, Chamwino, Chemba, Dodoma Jiji, Kondoa na Mpwapwa. Aidha vyama vikuu na vya ushirika vya masoko 32 vinatarajiwa kushiriki utekelezaji wa mfumo huo katika msimu wa mwaka 2025/2026.

Post a Comment