TIRDO YAFUNGUA UKURASA MPYA WA MAPINDUZI YA VIWANDA TANZANIA ‎

 


‎Na Edward Winchislaus

‎Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limeendelea kujiimarisha katika safari ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha teknolojia na ubunifu wa viwanda baada ya kutangaza mipango mikubwa ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Mpango huo umetajwa kuwa hatua muhimu ya kuharakisha uchumi wa viwanda unaotegemea maarifa, teknolojia na matumizi ya rasilimali za ndani.


‎Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara bungeni leo Mei 22, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Judith Kaping amesema TIRDO imeendelea kuelekeza nguvu katika tafiti za kisasa na ubunifu wa teknolojia kwa lengo la kuongeza thamani ya malighafi zinazopatikana nchini pamoja na kukuza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.


‎Katika mwaka huo wa fedha, TIRDO imepanga kuanzisha Kituo cha Taarifa za Viwanda (NIIMS), mfumo ambao unatarajiwa kusaidia ukusanyaji wa taarifa muhimu za viwanda, ubashiri wa teknolojia pamoja na kutoa viatamizi kwa wabunifu wa teknolojia nchini. Hatua hiyo imeelezwa kuwa chachu ya kuwasaidia vijana wabunifu kupata mazingira bora ya kukuza teknolojia zao na kuzifikisha sokoni.


‎Aidha, shirika hilo limepanga kufanya tafiti za mnyororo wa thamani wa madini adimu katika maeneo ya Kyerwa mkoani Kagera, Iramba mkoani Singida pamoja na Mpwapwa mkoani Dodoma. Tafiti hizo zinatarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji wa viwanda vinavyotumia madini hayo ambayo yanaendelea kuhitajika duniani katika uzalishaji wa vifaa vya kisasa vya teknolojia.


‎Katika kuimarisha ubora wa bidhaa za viwandani, TIRDO imeendelea kukamilisha ithibati za maabara pamoja na kuboresha maabara za kemia, makaa ya mawe, nguo na ngozi, nishati pamoja na mafuta na gesi. Serikali imeeleza kuwa maboresho hayo yataongeza uwezo wa ndani wa kufanya vipimo vya kisasa badala ya kutegemea huduma kutoka nje ya nchi.


‎Kwa upande wa nishati, shirika hilo limepanga kuanzisha maabara ya nishati na madini mkoani Njombe pamoja na maabara maalum ya upimaji wa majiko ya kupikia. Mpango huo umeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za taifa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na teknolojia rafiki kwa mazingira.


‎Katika hatua nyingine, TIRDO imepanga kujenga kiwanda darasa cha vifaa vya kielektroniki kitakachotumia malighafi zinazopatikana hapa nchini. Mradi huo unatajwa kuwa mwanzo wa safari ya Tanzania kuelekea uzalishaji wa vifaa vya teknolojia vinavyotengenezwa kwa kutumia rasilimali za ndani.


‎Pia shirika hilo limeendelea na maandalizi ya kujenga mtambo wa biogas asilia Jijini Dar es Salaam utakaobadilisha taka kutoka masoko ya Mabibo, Ilala Boma na Temeke Sterio kuwa gesi ya petroli iliyosindikwa (LPG). Mradi huo unatarajiwa kusaidia usimamizi wa taka mijini huku ukiwa chanzo mbadala cha nishati safi kwa wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post