Na Edward Winchislaus
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema imefanikiwa kuvuka lengo la utatuzi wa migogoro ya ardhi pamoja na kuongeza kasi ya utoaji wa hatimiliki nchini katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo Mei 28, 2026, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo amesema hadi Mei 15, 2026 jumla ya migogoro ya ardhi 5,573 imetatuliwa, sawa na kuvuka lengo la migogoro 3,000 lililowekwa kwa mwaka huo.
Dkt. Akwilapo amesema kati ya migogoro hiyo, 3,183 ilitatuliwa kupitia Kliniki za Ardhi huku mingine 2,390 ikitatuliwa kupitia utaratibu wa kawaida wa kiutawala.
“Katika mwaka 2026/2027, wizara imepanga kushughulikia migogoro 4,000 kiutawala. Natoa rai kwa viongozi, watumishi na wananchi kuzingatia sheria za ardhi, kanuni na miongozo ili kuepuka kuanzisha migogoro mipya,” amesema Dkt.Akwilapo.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema wizara imefanikiwa kuandaa na kusajili hatimiliki 107,683 hadi kufikia Mei 15, 2026, sawa na asilimia 21.54 ya lengo lililowekwa.
Aidha, amesema hati za hakimiliki ya kimila zilizotolewa zimefikia 99,762 sawa na asilimia 19.19 ya lengo, huku vyeti vya ardhi ya vijiji 148 vikitolewa sawa na asilimia 148 ya lengo.
Pia wizara imetoa hati za sehemu ya jengo 914 sawa na asilimia 91.4 ya lengo lililowekwa kwa mwaka huo wa fedha.Dkt. Akwilapo amesema mafanikio hayo yanatokana na jitihada za kuimarisha usimamizi wa ardhi nchini pamoja na kuongeza usalama wa umiliki wa ardhi kwa wananchi.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, wizara imejipangia kuandaa na kusajili hatimiliki 200,000, hati za hakimiliki ya kimila 300,000, vyeti vya ardhi ya vijiji 60, hati za sehemu ya jengo 1,000 pamoja na kusajili miamala ya hatimiliki na nyaraka za kisheria 100,000.

Post a Comment