Na Edward Winchislaus
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu),Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Serikali imeendelea kupata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kutokana na kuimarishwa kwa operesheni za udhibiti na ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Akizungumza leo Mei 29, 2026 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2025, Prof. Kabudi amesema kiasi cha bangi kilichokamatwa kimepungua kwa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka 2024 kutokana na uteketezaji wa mashamba makubwa ya bangi pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii.
Amesema katika mwaka 2025 jumla ya tani 1,017.26 za bangi zimekamatwa huku tani 26.36 za mirungi nazo zikikamatwa, hali ambayo imeonesha kuimarika kwa operesheni za ufuatiliaji na udhibiti katika maeneo ya mipaka na njia zinazotumika kusafirisha dawa hizo.
Prof. Kabudi amesema Serikali pia imefanikiwa kukamata dawa za kulevya za viwandani ikiwemo methamphetamine kilogramu 907.18, heroin kilogramu 672.23, cocaine kilogramu 4.89 pamoja na kiasi cha MDMA na MDA kilichokuwa kikiingizwa nchini kwa njia mbalimbali.
Aidha, amesema kwa mara ya kwanza Serikali imekamata tani 29.52 za dawa mpya ya kulevya aina ya Kratom iliyokuwa imeingizwa nchini ikidaiwa kuwa ni mbolea, lakini uchunguzi umebaini kuwa ilikuwa ni dawa ya kulevya hatari.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeendelea kuimarisha ukaguzi kwenye vituo vya forodha, kampuni za usafirishaji na biashara za kemikali bashirifu ambapo tani 31.76 za kemikali hizo pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya zimekamatwa katika operesheni mbalimbali zilizofanyika nchini.
Amesema mwaka 2025 jumla ya mashauri 1,124 ya dawa za kulevya yamefunguliwa mahakamani huku mashauri 1,373 yakitolewa hukumu na Jamhuri kushinda mashauri 1,058, hatua ambayo imeonesha kuimarika kwa usimamizi wa sheria dhidi ya wahusika wa biashara hiyo haramu.
Profesa Kabudi amesema Serikali imeendelea kutoa huduma za tiba na utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya ambapo watu 85,425 wamepata huduma kupitia hospitali za rufaa, kliniki za MAT pamoja na nyumba za upataji nafuu nchini kote.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya biashara na matumizi ya dawa za kulevya ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama na huru dhidi ya athari za dawa hizo.



Post a Comment