‎WIZARA YA ARDHI YAOMBA BILIONI 210.2 MWAKA 2026/27, YAPANGA KUHARAKISHA UPIMAJI NA UMILIKISHAJI ARDHI ‎

 


‎Na Edward Winchislaus

‎Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeomba kuidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni 210.2  kwa mwaka wa fedha 2026/27 ili kutekeleza vipaumbele mbalimbali ikiwemo kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi nchini.

‎Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo bungeni leo Mei 28, 2026, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo amesema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 100.2 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Sh.bilioni 110 zikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

‎Dk Akwilapo amesema katika mwaka huo wa fedha, wizara itatekeleza vipaumbele mbalimbali vinavyolenga kuboresha sekta ya ardhi, makazi na maendeleo ya miji ambapo amesema serikali itaongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi katika maeneo ya mijini, vijijini pamoja na maeneo ya kimkakati ili kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi.

‎Aidha, amesema wizara itaendelea kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji, kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma pamoja na ukusanyaji wa maduhuli ya sekta ya ardhi.

‎“Tutaimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na kuhakikisha uwepo wa nyumba bora kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema Dk Akwilapo.

‎Pia amesema serikali itaendelea kuimarisha mipaka ya kimataifa, kuendeleza miji ya mipakani pamoja na kuongeza upatikanaji wa ramani kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post