Wizara ya Ujenzi imetangaza kuendeleza utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya barabara, madaraja na usafiri wa haraka katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza msongamano wa magari katika majiji makubwa nchini na kuboresha huduma za usafiri mijini.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma leo Mei 20, 2026, Ulega amesema Serikali imejipanga kuendeleza miradi hiyo katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya pamoja na miji ya Pwani, Iringa na Singida. Akibainisha kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mpango mpana wa kuboresha mtandao wa usafiri wa mijini unaokua kwa kasi kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.
Katika Jiji la Dar es Salaam, Serikali itaendelea na utekelezaji wa awamu mbalimbali za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT). Ulega amesema Awamu ya Tatu itahusisha ujenzi wa njia kutoka Maktaba hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kupitia Gongolamboto yenye urefu wa kilomita 23.3. Aidha, Awamu ya Nne itajumuisha njia za Maktaba–Morocco, Mwenge–Tegeta pamoja na Mwenge–Ubungo zenye jumla ya kilomita 30.1.
Waziri huyo ameongeza kuwa maandalizi ya Awamu ya Tano ya BRT kutoka Ubungo hadi Bandarini kupitia Tabata–Segerea na Tabata–Kigogo yenye urefu wa kilomita 27.6 yanaendelea sambamba na ujenzi wa daraja la juu la kupitisha magari katika eneo la Tabata. Serikali inaamini miradi hiyo itasaidia kupunguza muda wa safari kwa wakazi wa Dar es Salaam na kuongeza ufanisi wa mfumo wa usafiri wa umma.
Mbali na miradi ya BRT, Serikali pia inaendelea na maandalizi ya Mpango Kabambe wa Usafiri wa Haraka wa Tanzania (Tanzania Expressway Master Plan) kwa kushirikiana na Korea International Cooperation Agency. Mpango huo unalenga kuweka ramani na mwongozo wa kimkakati wa maendeleo ya barabara za haraka nchini ili kuendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya usafiri.
Ulega amesema Serikali pia inaendelea na utekelezaji wa miradi ya Expressway ikiwemo mradi wa Kibaha–Chalinze–Morogoro wenye urefu wa kilomita 163.8 ambao upo katika hatua za kumpata mwekezaji kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP). Aidha, maandalizi ya upembuzi yakinifu yanaendelea kwa miradi ya Expressway katika barabara ya Nyerere kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam hadi Uwanja wa Ndege, barabara za Mandela na Sam Nujoma kutoka Mfugale hadi Mwenge pamoja na mradi wa KIA hadi Arusha.

Post a Comment