‎MBUNGE MUTASINGWA AIPONGEZA SERIKALI KWA MAPINDUZI YA MIUNDOMBINU KAGERA,ATOA USHAURI WA KUMALIZA MADENI YA WAKANDARASI ‎

 ‎


Na Edward Winchislaus

‎Mbunge wa Bukoba Mjini,Mha. Johnston Mutasingwa, ameendelea kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa ya miundombinu yaliyotekelezwa mkoani Kagera, akisema wananchi wa mkoa huo sasa wameshuhudia maendeleo ambayo kwa miaka mingi yalionekana kuwa ndoto.


‎Akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi bungeni leo Mei 20, 2026, Mutasingwa amesema serikali imefanikiwa kujenga madaraja makubwa yaliyokuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu, likiwemo Daraja la Kyetema, ambalo limekuwa suluhisho muhimu kwa changamoto za usafiri na mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya Kagera.

‎Amesema kupitia uwekezaji huo, wananchi wameendelea kunufaika na huduma bora za usafiri huku shughuli za kiuchumi zikiongezeka kutokana na kuimarika kwa miundombinu ya barabara na madaraja. Aidha, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi nchini.

‎Mutasingwa amesema mfumo wa kuwapa kazi wakandarasi wa ndani umeendelea kusaidia fedha kubaki nchini sambamba na kukuza uwezo wa kampuni za Kitanzania. Amesema kwa sasa miradi mingi imekuwa ikigawanywa kwa makandarasi kadhaa wazawa ambao wameendelea kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

‎Katika Jimbo la Bukoba Mjini, mbunge huyo amesema ujenzi wa barabara ya njia nne eneo la Nyangoye umefikia hatua nzuri baada ya serikali kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Hata hivyo, ameomba madeni madogo ya mkandarasi aliyebaki yalipwe kwa wakati ili kukamilisha mradi huo ulioanza tangu mwaka 2023.

‎Mbali na hayo, Mutasingwa ameishauri serikali kulifanyia kazi Daraja la Kasalani lililopo katika barabara ya Bukoba Port kuelekea Kashai, akisema daraja hilo limeendelea kuleta changamoto kubwa wakati wa mvua kutokana na maji kujaa na kuzuia wananchi kupita kwa urahisi.

‎Pia ameishauri serikali kuipa TANROADS hadhi ya mamlaka kamili ili kuongeza ufanisi wa usimamizi wa barabara na vyanzo vya mapato. Aidha, amependekeza serikali kutafuta mfumo maalum wa kumaliza madeni ya wakandarasi kupitia taasisi moja ya kifedha, hatua ambayo amesema itasaidia kupunguza riba kubwa na kutoa nafasi kwa fedha za maendeleo kuendelea kutekeleza miradi muhimu nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post