SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAVUNJA REKODI UJENZI WA BARABARA ZA LAMI NA MADARAJA ‎



Na Edward Winchislaus

‎Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuandika historia katika sekta ya miundombinu baada ya kufanikisha ujenzi wa zaidi ya kilometa 1,495 za barabara kwa kiwango cha lami ndani ya kipindi cha miaka mitano. Mafanikio hayo pia yameambatana na ujenzi wa madaraja makubwa 18 yanayorahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.


‎Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Mei 20, 2026, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega alisema mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuboresha sekta ya uchukuzi na kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi kwa urahisi zaidi.


‎Waziri Ulega alieleza kuwa mtandao wa barabara za kitaifa unaosimamiwa na TANROADS umefikia kilometa 37,734.41, ambapo kilometa 12,225.26 tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami. Hatua hiyo imeelezwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa na huduma pamoja na kupunguza changamoto za usafiri kwa wananchi.




‎Amesema tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, nchi ilikuwa na kilometa 1,360 pekee za barabara za lami. Aidha, kuanzia Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi ya Tano zilijenga jumla ya kilometa 9,369.81 za barabara za lami, jambo linaloonyesha kasi kubwa ya utekelezaji wa miradi katika Serikali ya sasa.


‎Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza nguvu katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha biashara na kurahisisha huduma za kijamii kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.


‎Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara ya Ujenzi ilipanga kujenga na kukarabati kilometa 450 za barabara kuu na za mikoa kwa kiwango cha lami pamoja na kilometa 820 kwa kiwango cha changarawe. Hadi kufikia Aprili 2026, tayari kilometa 243.13 za barabara za lami na kilometa 94.36 za changarawe zilikuwa zimekamilika kujengwa na kukarabatiwa.


‎Kwa upande wa madaraja, Serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja tisa ikiwemo Mitomoni, Mirumba, Nzali, Doma, Chakwale, Nguyami, Mkili, Kalebe na Itembe, huku madaraja mengine 11 yakiendelea kujengwa. Serikali pia inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa madaraja 13 pamoja na kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa miradi mbalimbali ya madaraja nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post