Na Edward Winchislaus
Serikali imesema biashara ya asali ya Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika soko la kimataifa baada ya mauzo ya bidhaa hiyo nje ya nchi kuongezeka kwa kiwango kikubwa ndani ya mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri Ashatu Kijaji amesema Tanzania imeuza tani 1,596.8 za asali mwaka 2025 ikilinganishwa na tani 951.6 zilizouzwa mwaka 2024.
Amesema ongezeko hilo limeifanya sekta ya ufugaji nyuki kuendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato ya taifa kupitia biashara ya nje, huku mahitaji ya asali ya Tanzania yakiongezeka katika mataifa mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa Dkt. Kijaji, thamani ya mauzo ya asali pia imepanda kutoka shilingi bilioni 11.4 mwaka 2024 hadi kufikia shilingi bilioni 19.2 mwaka 2025, jambo lililoonyesha ukuaji mkubwa wa soko la bidhaa hiyo.
Waziri huyo amesema mafanikio hayo yametokana na hatua za Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya ufugaji nyuki pamoja na kuhakikisha wazalishaji wanazingatia ubora unaohitajika katika masoko ya kimataifa.
Aidha, amesema asali ya Tanzania imeendelea kufikia wastani wa asilimia 97 ya viwango vya ubora vinavyotakiwa na Umoja wa Ulaya kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, hali iliyoongeza ushindani wa bidhaa hiyo duniani.
Kutokana na ubora huo, Tanzania imeendelea kupata masoko mapya ya asali katika nchi mbalimbali zikiwemo Marekani, China, Falme za Kiarabu na kwa mara ya kwanza Uingereza.


Post a Comment