Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Ashatu Kijaji ameomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi bilioni 334.3 kwa ajili ya kutekeleza shughuli za Wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2026/27 huku Serikali ikiweka mkazo mkubwa katika kukuza utalii, uhifadhi wa maliasili na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
Akiwasilisha mpango na bajeti ya Wizara hiyo bungeni leo Mei 15,2026, Dkt. Kijaji amesema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 272.0 zitatumika kwa matumizi ya kawaida huku Shilingi bilioni 62.3 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Amesema fedha za maendeleo zitasaidia kuimarisha miundombinu katika maeneo ya utalii na hifadhi ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, mawasiliano pamoja na huduma za kijamii ili kuongeza ushindani wa sekta ya utalii nchini.
Katika bajeti hiyo, Serikali pia imepanga kuongeza nguvu katika utangazaji wa vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi kwa kutumia mikakati mahsusi ya masoko, hususan katika masoko mapya ya Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati.
Waziri huyo amesema Wizara imejipanga kuendeleza mazao mbalimbali ya utalii ikiwemo utalii wa meli, mikutano na matukio maalum (MICE), utalii wa michezo, tiba, anga pamoja na fukwe kwa lengo la kupanua fursa za ajira, uwekezaji na mapato ya Taifa.
Aidha, Serikali imeendelea kuweka msisitizo katika kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale kupitia ushirikishwaji wa jamii, matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na mapambano dhidi ya ujangili na uharibifu wa mazingira.
Dkt. Kijaji amesema Wizara pia imepanga kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni mbalimbali ili ziendane na mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya sekta hiyo.
Sambamba na hilo, amesema Serikali itaendelea kuimarisha utafiti, ubunifu na maendeleo ya rasilimaliwatu kwa kuongeza uwezo wa watumishi pamoja na taasisi za mafunzo ili kuongeza tija na uendelevu wa sekta ya maliasili na utalii nchini.

Post a Comment