Na Edward Winchislaus
Wizara ya Maliasili na Utalii imesema Shindano la Urembo la Dunia la Miss World 2027 litakuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii na urithi wa taifa.
Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha mashindano hayo yanatoa matokeo chanya kwa sekta ya utalii nchini.
Dkt. Kijaji amesema Serikali itaandaa ziara maalum za utalii na mafunzo (FAM Trip) kwa walimbwende pamoja na waandishi wa habari kutoka mataifa mbalimbali kabla ya mashindano hayo kufanyika.
Amesema ziara hizo zitawawezesha wageni kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, hatua itakayosaidia kuitangaza Tanzania kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii duniani kote.
Aidha, wizara hiyo imeeleza kuwa wadau wa utalii watahamasishwa kuandaa na kuuza vifurushi vya safari kupitia majukwaa ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), huku matangazo ya mashindano hayo yakitarajiwa kurushwa kupitia televisheni, redio, mitandao ya kijamii pamoja na tovuti mbalimbali za utalii.
Kwa mujibu wa Waziri Kijaji, washindi wa juu wa Miss World 2027 watapewa jukumu la kuwa mabalozi wa hiari wa kuitangaza Tanzania kimataifa ili kuongeza idadi ya watalii na kuifanya nchi kuwa kitovu cha utalii duniani.

Post a Comment