SEKTA YA UCHUKUZI YAIPA TANZANIA NGUVU YA MUUNGANIKO WA KIKANDA NA KIMATAIFA



‎Na Edward Winchislaus,Dodoma

‎Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha sekta ya uchukuzi kama nguzo muhimu ya muunganiko wa kikanda na kimataifa, baada ya kufanikisha miradi mikubwa ya reli, bandari, usafiri majini na anga ndani ya siku 100 za Kipindi cha Pili cha uongozi wake.

‎Akizungumza Februari 1, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Serikali imekamilisha taratibu za ufufuaji wa Reli ya TAZARA kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa uboreshaji kati ya Tanzania, Zambia na Kampuni ya CCECC ya China. Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa Juni 2026 na unalenga kuimarisha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, kukuza biashara ya kikanda na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji kwa nchi zisizo na bandari.

‎Prof. Mbarawa amesema huduma za reli ya SGR na MGR zimeendelea kuimarika, ambapo zaidi ya abiria 838,000 na tani zaidi ya 85,000 za mizigo zimesafirishwa, hali inayochochea biashara ya ndani na ya mipakani. Aidha, Serikali imepokea vichwa viwili vya treni na mabehewa 50 ya mizigo ili kuongeza uwezo na ufanisi wa reli.

‎Katika hatua nyingine, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza kujiendesha bila kutegemea ruzuku ya mishahara kutoka Serikali, sambamba na kuanzishwa kwa Kampuni Tanzu ya TANRAIL yenye lengo la kuongeza mapato na ufanisi wa uendeshaji wa reli. Ujenzi wa reli ya SGR Dar es Salaam–Mwanza unaendelea, huku kipande cha Dar es Salaam–Dodoma kikiwa tayari kinahudumia abiria na mizigo.

‎Kwa upande wa bandari, Prof. Mbarawa amesema Serikali imeanza maandalizi ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, hatua zinazoongeza ushindani wa bandari za Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na kuchangia ongezeko la mapato ya TPA na TRA kwa mamia ya mabilioni ya shilingi.

‎Katika sekta ya usafiri majini, Serikali imezindua meli ya MV New Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, pamoja na kununua boti za uokoaji na Ambulance Boat kwa ajili ya kuimarisha usalama na huduma za dharura katika Ziwa Victoria.

‎Kwa sekta ya anga, Waziri Mbarawa amesema kukamilika kwa Jengo la Viongozi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere pamoja na kuongezwa kwa vituo vipya vya kimataifa kupitia ATCL kumeongeza muunganiko wa Tanzania na masoko ya kimataifa, hivyo kukuza biashara, utalii na uwekezaji.

‎Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya uchukuzi ili kuiweka Tanzania katika nafasi ya kimkakati ya usafirishaji kikanda na kimataifa.






Post a Comment

Previous Post Next Post