‎MAANDALIZI YA UTEKELEZAJI WA DIRA 2050 YAKAMILIKA,MIPANGO KUWASILISHWA BUNGENI FEB.2,2026

 



‎Na Edward Winchislaus,Dodoma.

‎ Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango (NPC) imetangaza kukamilika kwa maandalizi muhimu ya kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hatua inayotajwa kuwa ya kihistoria katika mwelekeo wa maendeleo ya Taifa kwa miongo ijayo.

‎Kwa mujibu wa NPC, utekelezaji wa Dira 2050 utaanza rasmi  Julai Mosi 2026, sambamba na kuanza kwa mwaka wa fedha 2026/2027, baada ya kukamilika kwa nyaraka kuu za mipango zitakazowezesha utekelezaji wake.

‎Akizungumza na waandishi wa habari leo Feburuali mosi,2026  jijini Dodoma Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, amesema kuwa Tume imekamilisha kuandaa nyaraka tatu muhimu ambazo ni Mpango Elekezi wa Muda Mrefu (2026/2027–2050/2051), Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/2027–2030/2031) pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2026/2027.

‎Amesema mipango hiyo imepitia ngazi zote za uamuzi Serikalini na inatarajiwa kuwasilishwa mbele ya Bungeni jijini Dodoma Februari 2,2026, ambapo  itajadiliwa na wabunge kwa wiki nzima.

‎“Uwasilishaji wa mipango hii ni hatua muhimu katika safari ya utekelezaji wa Dira 2050, ambayo inalenga kuijenga Tanzania yenye ustawi wa pamoja, ushindani wa kiuchumi na maendeleo jumuishi,” amesema Dkt. Msemwa.

‎Akizungumza kuhusu maandalizi ya utekelezaji, Dkt. Msemwa amesema NPC imeandaa Muongozo wa Upangaji wa Mipango ya Taifa  ili kuhakikisha Wizara, Idara, Taasisi za Umma pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaelewa na kuzingatia mwelekeo wa Dira 2050 katika mipango yao.

‎Katika hatua nyingine, NPC ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miradi (NPMIS), unaolenga kuimarisha uwajibikaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa kuzingatia matokeo.

‎“Dira ya 2050 imebeba matumaini ya Watanzania wote. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kufahamu mwelekeo wa Taifa letu na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mustakabali wa Tanzania,” amesema.

‎Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ilizinduliwa rasmi tarehe 17 Julai 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni dira inayolenga kulifikisha Taifa katika maendeleo ya juu, ustawi wa watu na mshikamano wa kitaifa ifikapo mwaka 2050.





Post a Comment

Previous Post Next Post