Na Edward Winchislaus,Dodoma.
Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua za makusudi kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuhakikisha haki inatendeka kwa uadilifu na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 2, 2026 na Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli jijini Dodoma ambapo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu, kuimarisha rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama na kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi, ikiwemo ujenzi wa Mahakama za Mwanzo katika kata zote zisizo na Mahakama za Mwanzo.
Pia amesisitiza kuwa uhuru wa Mahakama haupaswi kutumiwa kama kinga ya uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki, bali uwe nyenzo ya kutenda haki kwa kuzingatia Katiba, sheria za nchi na misingi ya uwazi na uadilifu.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewataka viongozi, wanasiasa na wananchi kuheshimu tume iliyoundwa na Rais kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuacha kuyajadili masuala hayo nje ya mifumo ya kisheria.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, ametangaza kuwa Mahakama imetunga kanuni mpya zitakazowezesha mashauri yenye masuala magumu ya kisheria, kikatiba na kiushahidi kusikilizwa na jopo la majaji watatu ili kuongeza ufanisi na ubora wa maamuzi ya Mahakama.
Aidha,amesema Mahakama imeimarisha haki ya dhamana kwa watuhumiwa wenye sifa za kisheria kuanzia ngazi za chini, ikiwemo Mahakama za Mwanzo, ambapo maombi ya dhamana yataamuliwa siku hiyo hiyo ili kupunguza ucheleweshaji wa haki na mianya ya rushwa.
Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amewataka viongozi kuwa waangalifu na kauli zao, akisisitiza kuwa Taifa lipo katika kipindi nyeti kinachohitaji busara, hekima na maneno ya kuunganisha wananchi.
Mwabukusi amesema uwajibikaji ni msingi wa kurejesha imani na matumaini ya wananchi kwa Taifa, akisisitiza kuwa changamoto zilizojitokeza kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 zinapaswa kushughulikiwa kwa haki, uwazi na kwa masilahi mapana ya Taifa.







Post a Comment