Na Suzana Alex
MGOMBEA wa Ubunge wa Jimbo la Dodoma kipitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Paschal Chinyele amewashauri wananchi kutowachagua wagombea wa vyama vya siasa kwa mazoea na kwa ushabiki badala yake watumie nafasi hiyo kuchagua viongozi watakaowavusha na kuwapelekea kwenye maendeleo.
Chinyele amesema hayo alipokuwa akiomba kura kwa wakazi wa Kata ya Hazina Dodoma kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa mtaa wa Hazina.
Kwenye ushauri wake huo,amewataka wananchi kutumia fursa hiyo muhimu ya uchaguzi mkuu kutofanya makosa,bali wachague viongozi ambao wanaoona watawavusha kwa ajili ya maendeleo badala ya kuchagua kwa kufuata mkumbo,mazoea na kwa ushabiki.
"Hivyo niwaombe chagueni Chama ambacho kitakachoendelea kuwaletea mafanikio makubwa ya kimaendeleo,na kitakachojali watu wake bila kubagua kwa itikadi yoyote"alisema
Katika hatua nyingine mgombea huyo amewataka Watendaji wa serikali za mitaa,kuacha tabia ya kuwalipisha fedha wananchi pale wanapofika ili kupatiwa huduma.
Akifafanua amesema kuwa wananchi hao wamekuwa wakifika kwenye ofisi hizo za watendaji wanapohitaji huduma hutozwa fedha ili wahudumiwe suala ambalo linaweza kuwafanya kuichukia serikali yao iliyopo madarakani.
"Niwaombe watendaji msiwatoze wananchi kwa kuwaomba fedha bali muwahudumie,fanyenyi kazi zenu kama mlivyoapa,na mimi mkinichagua nitahakikisha suala hilo linapata ufumbuzi"amesema Chinyele
Mgombe huyo pia amesema wananchi wakimchagua atahakikisha makundi ya akina mama,vijana na watu wenye ulemavu wanaondokana na mikopo ya kausha damu.

Post a Comment