Na Edward Winchislaus.
Mgombea udiwani kupitia chama cha mapinduzi CCM,Kata ya Kilimani Jijini Dodoma Mhe.Musa Mkunda ameahidi kutatua changamoto ya miundombinu katika kata hiyo iwapo atapewa ridhaa na wananchi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.2025.
Mkunda ameahidi hayo Septemba 14.2025 wakati wa ufunguzi wa kampeni zake kwenye kata hiyo ambapo amebainisha kuwa changamoto kubwa inayo wakumba wananchi wa eneo hilo ni pamoja na uwepo wa miundombinu mibovu ya maji taka huku akiahidi kuwa akipata ridhaa ya kuwa diwani ataitatua.
"Mheshimiwa Chinyere hadhara hii yote imeahidi kukupa kura namimi nikiamini unaenda kuwa mbunge wa Dodoma mjini,sisi kata ya kilimani tunachangamoto kubwa ya miundombinu naomba hili mimi na wewe twende nalo kwa miguu miwili ili tuweze kulitatua likiwemo suala la maji taka,"amesema.
Aidha mgombea udiwani huyo ametumia jukwaa hilo kumnadi na kumuombea kura mgombea urais kupitia chama cha mapinduzi CCM Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake mgombea ubunge katika jimbo la Dodoma mjini kupitia tiketi ya CCM Mhe.Pascal Chinyere amesema tayari serikali imekwisha anzisha mradi wa kujenga bomba kubwa katika eneo la swaswa ili kusukuma maji taka yote yanayo wakumba wakazi wa kata ya kilimani.
Pia amesema iwapo watawapa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo wataiomba serikali kuwapatia eneo la kujenga kituo cha Afya katika kata hiyo ili kuwasaidia wananchi wa kata hiyo wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma za Afya.




Post a Comment