Mkurugenzi wa Mashtaka ambae pia ni mlezi wa chama cha Mashtaka SACCOS Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka wanachama wa chama hicho kuwa na nidhamu ya fedha ili wanapokopa mikopo yao waweze kurudisha fedha hizo kwa wakati.
Wito huo ameutoa leo tarehe 11 Septemba, 2025 Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa kawaida wa chama hicho uliyokuwa na lengo la kupitia, kuidhinisha maboresho ya sera za chama hicho pamoja na kujadili, kupitisha mipango ya utekelezaji ya chama hicho.
“Niwatake muwe na nidhamu ya kifedha, mikopo tunayoichukua tuirudishe kwa wakati ili tuendelee kuimarisha SACCOS yetu na tusikope pasipo kuwa na lengo hakikisha ukikopa kuwa na lengo la kuzifanyia kazi fedha hizo." Amesema Mkurugenzi wa Mashtaka.
Pia amewasihi watumishi hao kuitumia SACCOS hiyo kwa kufanya maendeleo kwani ipo mikopo ya maendeleo, ipo mikopo ya dharura hivyo kupitia SACCOS hiyo wanaweza kujenga hata nyumba.
Pamoja na hayo aliwataka wanachama hao kuongeza bidii ya kuweka akiba kwani wakiwa na akiba kubwa watajiongezea kiwango cha kukopa zaidi kwakuwa wameweka mpango wa kukopesha hadi milioni 50 kutoka milioni 20.
Aidha amewakumbusha viongozi wa chama hicho kuzingatia misingi ya uadilifu na uwajibikaji ili kuepukana na migogoro inayoweza kujitokeza ndani ya chama hicho.
“Vongozi sitaki kusikia tuhuma zozote za matumizi mabaya ya fedha za chama hiki, SACCOS hii natamani iwe bora na hatujafunga mipaka watumishi wa Taasisi nyingine za serikali kujiunga na SACCOS hii." Amesisitiza Mkurugenzi Mwakitalu.
Sambamba na hilo amewapongeza wanachama wa Mashtaka SACCOS kwa kuendelea kudumisha umoja, kuimarisha mtaji wa SACCOS hiyo na kutoa mkopo wa riba nafuu kwa wanachama wa chama hicho huku akiwataka watumishi wengine wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mbao bado hawajajiunga katika SACCOS hiyo kuhakikisha wanajiunga ili wapate mikopo yenye riba nafuu.
Kwa upande wake Afisa Utumishi Mkuu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bw. Mashaka Pascal Mayala amesema SACCOS hiyo ilianzishwa ili kuzuia mikopo ya kausha damu kwa watumishi wa ofisi hiyo ambapo ameeleza kuwa SACCOS hiyo huwapatia mikopo yenye riba nafuu.
“Viongozi wetu wanayo dira ya kutuwezeha sisi watumishi kuwa na kipato bora ili kuzuia kupata mikopo ya kausha damu, licha ya kwamba tulianza kusuasua ila kwa kila mmoja anaifurahia SACCOS hii na kabla ya chama hiki kuanzishwa tulikuwa tukikopa benki na riba inakuwa kubwa sawa na kiasi ulicho kikopa." Amesema Afisa Mkuu.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo na hali ya utekelezaji wa chama hicho, Mwenyekiti wa Mashtaka SACCOS Bw. Juma Katanga amesema chama hicho kilianza kikiwa na wanachama 37 mwaka 2022 ambapo kwa sasa kimefikisha wanachama 990 huku kikitoa mikopo zaidi ya shilingi bilioni Moja kutoka mikopo ya milioni 5.6 mwaka 2023.
Ameongeza kuwa kati ya mikopo hiyo iliyotolewa kiasi cha shilingi milioni 500 ndicho kilicho rejeshwa huku shilingi bilioni 1.2 zikiwa bado kwa wanachama hao.
“Idadi ya wanachama kwa mwaka 2022 tulikuwa na wanachama 37 mwaka 2023 wakafikia 247, mwaka 2024 wakafikia 450 na hadi kufikia jana Septemba 10, 2025 tunaidadi ya wanachama 990, na hii ni baada vya wengine kuhama.
“Suala la mikopo mwaka 2022 hatukuwa na mikopo mwaka 2023 ilitolewa mikopo ya milioni 5.6, mwaka 2024 ilitolewa mikopo ya milioni 354.7 mwaka 2025 imetolewa jumla ya mikopo bilioni 1,764,528." Amefafanua Bw. Katanga.

Post a Comment