Na Edward Winchislaus.
Serikali imeeleza kuwa sekta ya ushirika imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku ikisisitiza kuwa itaendelea kuwekeza katika kuimarisha vyama vya ushirika ili kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi jumuishi na kuinua maisha ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 5, 2026, jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter Msoffe, alipokuwa akifungua Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo. Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 6 na yamebeba kaulimbiu isemayo "Ushirika kwa Dunia Yenye Amani."
Prof. Msoffe amesema ushirika umeendelea kuwa daraja muhimu la kuwawezesha wananchi kupata pembejeo za kilimo, elimu ya kilimo na huduma nyingine zinazochochea uzalishaji, akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha sekta hiyo kupitia maboresho ya mifumo ya TEHAMA na hatua nyingine za kiutawala.
Amesema Chuo cha Ushirika Moshi kimeendelea kupanua programu za mafunzo ili kuongeza wataalamu wenye uwezo wa kusimamia maendeleo ya sekta hiyo, huku serikali ikiwa imetoa shilingi trilioni 1.2 kupitia mikopo kwa vyama vya ushirika kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji na uwekezaji.
Aidha, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imelenga sekta binafsi kuchangia asilimia 70 ya pato la taifa, ambapo vyama vya ushirika vimeendelea kuwa miongoni mwa wadau wakuu wa kufanikisha lengo hilo. Ameongeza kuwa serikali imeendelea kuhamasisha vijana, wanawake na makundi mengine kujiunga na ushirika sambamba na kuimarisha misingi ya utawala bora.
Hata hivyo, Prof. Msoffe amesema ushiriki mdogo wa vijana pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi zimeendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta hiyo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kuzitafutia ufumbuzi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema juhudi za kuendelea kuboresha sekta ya ushirika zimeifanya kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa, akieleza kuwa ushirika imara umeendelea kujenga uchumi imara, kuleta ustawi wa wananchi na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Tito Haule, amewataka washiriki wa maadhimisho hayo kutoka mikoa mbalimbali nchini kutumia kongamano hilo kujadili kwa kina fursa na changamoto zinazoikabili sekta ya ushirika ili kuweka mikakati itakayoongeza mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Maadhimisho hayo yameendelea kuwa jukwaa la wadau wa ushirika kutathmini mafanikio, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuifanya sekta hiyo kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania na ustawi wa wananchi.



Post a Comment