Na Edward Winchislaus.
Serikali imeahidi kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta ya ushirika nchini, ikiwemo maboresho ya sera, mfumo wa kodi na masoko ya mazao ya kimkakati, huku ikisisitiza kuimarishwa kwa uwajibikaji na uadilifu ili kuongeza mchango wa vyama vya ushirika katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, kwa niaba ya Waziri Mkuu, wakati akifunga kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika leo Julai 6, 2026 jijini Dodoma. Maadhimisho hayo, ambayo ni ya 24 tangu yaanze kuadhimishwa nchini Tanzania, yameongozwa na kaulimbiu isemayo "Ushirika kwa Dunia Yenye Amani."
Silinde amesema Serikali imepokea hoja zote zilizowasilishwa na wanaushirika na itaendelea kuzifanyia kazi kwa lengo la kuondoa changamoto zinazoikwamisha sekta hiyo. Amesema Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, kuongeza thamani ya mazao na kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vya ubadhirifu vinavyodhoofisha imani ya wanachama.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema zaidi ya vyama 6,000 vya ushirika vimesajiliwa nchini. Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto za usimamizi na uaminifu, huku akieleza kuwa TCDC inaendelea na mikakati ya kupeleka ushirika katika sekta za kimkakati, ikiwemo sekta ya madini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter Msoffe, amesema Serikali itaendelea kuunga mkono sekta ya ushirika ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua uchumi wa wananchi.
Akiwasilisha risala ya wanaushirika, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Tito Haule, amesema zaidi ya Watanzania milioni 3.4 ni wanachama wa vyama vya ushirika, huku AMCOS zikiongeza mauzo kutoka shilingi trilioni 1 hadi trilioni 3 katika mwaka wa fedha 2024/2025. Amesema vyama vya ushirika vimeanzisha zaidi ya viwanda 400 vya kuongeza thamani ya mazao na kutoa ajira zaidi ya 156,000.
Haule amesema pamoja na mafanikio hayo, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ushuru mkubwa unaotozwa kwa vyama vya ushirika, changamoto za masoko ya mazao ya kimkakati, ucheleweshaji wa malipo ya wanachama na baadhi ya bodi za mazao kusajili madalali wanaorudisha nyuma maendeleo ya ushirika.
Kutokana na changamoto hizo, wanaushirika wameiomba Serikali kuhuisha Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002 pamoja na kufanya maboresho ya mfumo wa kodi kwa kupunguza kodi ya mapato ya vyama vya ushirika kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 ili kuongeza ufanisi na uwezo wa vyama hivyo kuwahudumia wanachama wake.
Akihitimisha maadhimisho hayo, Silinde amewataka viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika kuendelea kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na mshikamano, sambamba na kuwashirikisha vijana na wanawake katika shughuli za ushirika, akisisitiza kuwa ushirika utaendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa Taifa.





Post a Comment