Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi, amani na utendaji wa vyombo vya ulinzi nchini.
Wizara hiyo ikiongozwa na Waziri wake Dkt. Rhimo Nyansaho imeomba jumla ya shilingi trilioni 4.286, ambapo trilioni 3.86 ni matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 426.53 ni kwa ajili ya maendeleo.
Aidha, Dkt. Nyansaho amesema Serikali itaendelea kuliimarisha jeshi kwa zana za kisasa, teknolojia, mawasiliano pamoja na rasilimali watu ambapo serikali imepanga kuboresha mazingira ya kazi kwa wanajeshi, ikiwemo huduma za afya, makazi, mafunzo, mazoezi pamoja na maslahi yao.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuboresha miundombinu ili liweze kupokea vijana wengi zaidi kwa mafunzo ya kijeshi na stadi za kazi.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imepanga kuanzisha viwanda vipya vya sekta ya ulinzi vitakavyozalisha bidhaa za matumizi ya kijeshi na kiraia kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Pia amesema Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya ulinzi pamoja na kushirikiana na mamlaka za kiraia kukabiliana na majanga na dharura mbalimbali nchini.

Post a Comment