‎WAHITIMU WA JKT WAASWA KUWA WAZALENDO

 


Na Edward Winchislaus

‎Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amewataka vijana wanaopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutumia stadi wanazozipata kujiajiri, kujitegemea na kuwa raia wema.


‎Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma leo Mei 19, 2026, Dkt. Nyansaho amesema mafunzo ya JKT yameendelea kuwajengea vijana uzalendo, ukakamavu, umoja wa kitaifa pamoja na stadi mbalimbali za maisha na kazi.


‎“Nitoe rai kwa vijana wote wanaopata fursa ya mafunzo hayo kuwa raia wema na kuzitumia stadi walizozipata kujiajiri na kujitegemea,” amesema Dkt. Nyansaho.


‎Aidha, amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya kambi za JKT ambapo hadi mwaka wa fedha 2025/2026 kambi hizo zilikuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya vijana 60,000.


‎Kwa mujibu wa Waziri huyo, mpango uliopo ni kuendelea kufungua kambi mpya na kuboresha zilizopo ili JKT iweze kuchukua vijana 140,000 ifikapo mwaka 2031.


‎Mafunzo hayo hufanyika katika makundi mawili ambayo ni Kundi la Kujitolea na Kundi la Lazima kwa vijana wanaohitimu Kidato cha Sita katika kambi mbalimbali za JKT.

Post a Comment

Previous Post Next Post