Na Edward Winchislaus
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema katika Mwaka wa Fedha 2026/27 inatarajia kuajiri watumishi wapya 10,919 sambamba na kutekeleza maeneo nane ya vipaumbele yaliyolenga kuimarisha usalama, huduma za uraia na matumizi ya teknolojia nchini.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo Mei 25,2026, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amesema ajira hizo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ufanisi katika vyombo vya usalama vilivyo chini ya wizara.
Amesema kati ya watumishi hao wapya, makao makuu ya wizara yataajiri watumishi 249 huku Jeshi la Polisi Tanzania likitarajia kuajiri askari 8,040. Aidha, Jeshi la Magereza Tanzania litaajiri watumishi 1,046 na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji litapata watumishi 500.
Kwa upande mwingine, Idara ya Uhamiaji Tanzania inatarajia kuajiri watumishi 1,000 huku Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ikipanga kuajiri watumishi 84 ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Katika bajeti hiyo, Waziri Katambi amesema wizara itaendelea kuboresha miundombinu ya vyombo vya usalama ikiwemo makazi ya maofisa, wakaguzi, askari pamoja na watumishi wasio askari ili kuongeza mazingira bora ya kazi na utendaji.
Pia wizara imepanga kuendelea kuboresha upatikanaji wa vitendea kazi ikiwemo vyombo vya usafiri na usafirishaji kwa taasisi zote zilizo chini yake, hatua inayolenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu ya kiusalama nchini.
Katambi amesema wizara itaendelea kufanya tafiti mbalimbali kubaini sababu za kuongezeka kwa makosa mapya pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuyadhibiti, huku matumizi ya TEHAMA yakipewa kipaumbele katika utoaji wa huduma na usimamizi wa shughuli zake.
Aidha, wizara imepanga kuwajengea uwezo watumishi na askari kupitia mafunzo mbalimbali ya kitaaluma na kiutendaji ili kuongeza weledi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Katika miradi ya maendeleo, wizara itaanza ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) jijini Dodoma pamoja na ofisi 31 za usajili za wilaya, kituo cha mafunzo na matengenezo ya vifaa vya TEHAMA mjini Kibaha na nyumba salama kwa waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu jijini Dar es Salaam. Wizara pia imesema itaendelea kuimarisha shughuli za uzalishaji mali kupitia kilimo, mifugo, viwanda na utunzaji wa mazingira.


Post a Comment