‎SERIKALI:WANAWAKE BADO HAWANA NGUVU YA MAAMUZI YA KIUCHUMI NA KIJAMII

 


‎Na Edward Winchislaus

‎Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima amesema bado kuna changamoto kubwa ya wanawake kukosa nguvu ya kufanya maamuzi ya kiuchumi, kijamii na kimazingira licha ya jitihada mbalimbali za kuwawezesha wanawake nchini.

‎Akizindua matokeo ya Tafiti za Uwezeshaji wa Wanawake na Lishe 2023/24 pamoja na Utafiti wa Jinsia na Mazingira 2025 Mei 6, 2026 jijini Dodoma, Dkt. Gwajima alisema tafiti hizo zinaonesha wanawake wengi bado hawajiamini kushiriki katika maamuzi muhimu yanayohusu fedha, mali, ndoa, uzazi na matumizi ya rasilimali za mazingira.

‎Amesema ni asilimia 26 pekee ya wanawake wanaoamini kuwa mwanamke anapaswa kuwa huru kufanya maamuzi kuhusu shughuli zake za kiuchumi, huku asilimia 34.1 tu wakikubali mwanamke kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu ndoa, talaka na uzazi.


‎“Takwimu hizi zinaonesha bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kuongeza elimu na uhamasishaji kuhusu haki za wanawake na usawa wa kijinsia,” amesema Dkt. Gwajima.

‎Aidha, amesema zaidi ya nusu ya wanawake nchini bado hawana ushawishi katika matumizi ya fedha ndani ya familia, ambapo wanaume wanaongoza kwa asilimia 54.8 ya maamuzi ya kifedha ikilinganishwa na wanawake wenye asilimia 39.6.


‎Kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake wengi hushiriki katika vikundi vya kijamii visivyo rasmi kama vikoba na vikundi vya dini, lakini ni asilimia tisa tu wanaojihisi kusikilizwa katika jamii tofauti na wanaume ambao ni asilimia 26.

‎Katika upande wa lishe, Waziri huyo amesema utafiti umebaini kuwa mwanamke aliyewezeshwa kiuchumi ana nafasi kubwa ya kuboresha lishe ya familia yake.

‎Kwa upande wa mazingira, amesema wanawake ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na majukumu yao ya kila siku ikiwemo kutafuta kuni na maji.

‎“Asilimia 82.9 ya wanawake wameathiriwa na angalau athari moja ya mabadiliko ya tabianchi, huku ukame ukiwa changamoto kubwa zaidi hasa maeneo ya vijijini,” amesema.

‎Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kupitia elimu, mikopo, umiliki wa mali, ushiriki katika maamuzi pamoja na matumizi ya takwimu sahihi katika kupanga maendeleo.

‎Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Amina Msengwa amesema tafiti hizo zitasaidia katika kupanga sera na mipango yenye kuzingatia usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi nchini.




Post a Comment

Previous Post Next Post