‎HUDUMA ZA UPANDIKIZAJI VIUNGO ZAWAREJESHEA WATANZANIA MATUMAINI YA MAISHA

 


‎Na Edward Winchislaus

‎Huduma za upandikizaji viungo nchini Tanzania  kuonesha mafanikio makubwa, huku zikitoa matumaini mapya kwa wagonjwa waliokuwa wakikabiliwa na magonjwa sugu ya figo na damu.

‎Akizungumza leo Mei 06,2026 Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa kimataifa wa huduma za upandikizaji viungo nchini‎ ulioandaliwa na Hospitali ya kanda ya Benjamin Moapa (BMH)  na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema taifa limepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubigwa bobezi.



“Kwa sasa tunafanya upandikizaji wa figo na uloto hapa nchini, na tayari zaidi ya wagonjwa 147 wamepandikizwa figo kwa mafanikio,” amesema Dkt. Magembe.

‎Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha huduma hizo na inalenga kuanza upandikizaji wa ini na moyo, huku akihimiza wananchi kujiunga na bima ya afya ili kumudu gharama za matibabu hayo.



‎Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amesema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji wa serikali pamoja na ushirikiano wa wataalamu wa afya kutoka ndani na nje ya nchi.

‎“Lengo la mkutano huu ni kubadilishana uzoefu na kuimarisha zaidi huduma za kibingwa na ubingwa bobezi hapa nchini,” amesema Prof. Makubi.

‎Wakati huo huo, baadhi ya wanufaika wa huduma hizo wameeleza namna zilivyobadilisha maisha yao. Richard Masimba, aliyepandikizwa figo miezi sita iliyopita, alisema matibabu hayo yamemrejeshea afya na matumaini mapya.

‎Naye Naira Gwota, aliyefanyiwa upandikizaji uloto kutokana na ugonjwa wa selimundu, alisema hali yake imeimarika kwa kiasi kikubwa na sasa anaendelea vizuri na masomo yake baada ya kupona.

‎"kabla ya hiduma hii nilikuwa  naugua sana hadi kufikia hatua ya kukosa masomo kwasababu nilikuwa nalazwa sana Hospitali kila wakati",amesimulia.


Post a Comment

Previous Post Next Post