SERIKALI KUPANUA ELIMU YA UFUNDI NA AI, WANAFUNZI 374,000 KUNUFAIKA ‎

 


‎Na Edward Winchislaus

‎Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeweka mkazo mkubwa katika kupanua elimu ya ufundi, mafunzo ya ufundi stadi pamoja na teknolojia ya Akili Unde (AI), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na baadaye nchini.

‎Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma leo Mei 7, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amesema Serikali itaendelea kuongeza vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi sambamba na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka.

‎Profesa Mkenda amesema Serikali imesajili jumla ya vyuo 263 vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ambapo 45 ni vya elimu ya ufundi, 152 vya mafunzo ya ufundi stadi na 66 ni shule za sekondari za amali. Hatua hiyo imeifanya Tanzania kuwa na jumla ya taasisi 577 za elimu ya ufundi, vyuo 1,066 vya mafunzo ya ufundi stadi pamoja na shule 267 za sekondari za amali nchini.



‎Katika mwaka wa fedha ujao, Serikali inapanga kudahili wanafunzi 374,000 katika programu mbalimbali za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, huku lengo likiwa ni kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kuajirika kupitia ujuzi wa kisasa unaohitajika katika uchumi wa viwanda na teknolojia.

‎Sambamba na hilo, Serikali imeanzisha mpango maalum wa ufadhili wa masomo ya Akili Unde unaojulikana kama Samia Scholarship Extended, DS/AI+, utakaowawezesha vijana wa Kitanzania kusoma nje ya nchi katika vyuo vinavyotoa mafunzo ya kisasa ya teknolojia kwa kushirikiana na kampuni kubwa za teknolojia duniani. Kwa kuanzia, wanafunzi 50 waliofanya vizuri zaidi katika tahasusi za sayansi zenye masomo ya hisabati kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka 2025 wamechaguliwa kunufaika na ufadhili huo.

‎Mbali na uwekezaji katika elimu ya ufundi na teknolojia, Serikali pia imepanga kuboresha miundombinu ya elimu nchini kwa kujenga madarasa 1,360 ili kuimarisha utekelezaji wa sera ya elimu ya miaka 10 ya lazima pamoja na kuongeza mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari.

‎Aidha, Serikali itajenga mabweni 17 katika shule za sekondari 17, nyumba 33 za walimu pamoja na vituo 50 vya walimu katika halmashauri mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza motisha kwa walimu na kuinua ubora wa huduma za elimu nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post