‎SERIKALI KUFUNGUA FURSA KWA VIJANA 22,500 WALIOKOSA ELIMU RASMI ‎


Na Edward Winchislaus

‎Serikali imesema itaongeza idadi ya vijana wanaonufaika na Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Mfumo Rasmi kutoka 16,732 mwaka 2026 hadi kufikia vijana 22,500 mwaka 2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwapa elimu, ujuzi na stadi za maisha zitakazowasaidia kujiajiri na kuajiriwa.

‎Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma leo Mei 7, 2026.

‎Profesa Mkenda amesema Serikali inaendelea kuimarisha elimu nje ya mfumo rasmi kwa lengo la kuwafikia vijana na watu wazima waliokosa nafasi katika mfumo rasmi wa elimu kutokana na sababu mbalimbali, ili nao wapate maarifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira na maisha ya kila siku.

‎Amesema mpango huo unalenga kujenga jamii yenye watu wenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia elimu na mafunzo ya vitendo.

‎Katika bajeti hiyo, Waziri Mkenda pia ameliomba Bunge kuidhinisha shilingi trilioni 2.398 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Post a Comment

Previous Post Next Post