Na Edward Winchislaus
Wabunge wa Viti Maalum wanaowakilisha watu wenye ulemavu wameiomba Serikali kuongeza uwekezaji katika elimu jumuishi kwa kuingiza rasmi lugha ya alama kwenye mitaala ya shule pamoja na kuboresha huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu nchini.
Wakichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2026/2027 bungeni jijini Dodoma leo Mei 8, 2026, wabunge hao wamesema hatua hiyo itarahisisha mawasiliano na kuongeza usawa wa upatikanaji wa elimu kwa watu wenye ulemavu, hususan wenye uziwi.
Mbunge wa Viti Maalum wa kundi la wenye ulemavu, Stella Ikupa (CCM), amesema lugha ya alama inapaswa kufundishwa kama masomo mengine ya kawaida ili kila Mtanzania aweze kuwasiliana na watu wenye changamoto ya kusikia bila kutegemea wakalimani kila wakati.
Amesema watu wenye ulemavu wa kusikia hukumbana na changamoto kubwa wanapohitaji huduma katika maeneo mbalimbali kama vituo vya polisi, hospitali, saluni na ofisi kutokana na uhaba wa watu wanaofahamu lugha ya alama.
“Endapo kila mtu atafahamu lugha ya alama, mawasiliano yatakuwa rahisi zaidi kwa watu wenye ulemavu wa kusikia,” amesema Ikupa.
Mbunge huyo pia ameishauri Serikali kuwapa mafunzo ya elimu maalumu walimu wote nchini ili waweze kuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu badala ya kutegemea kundi dogo la walimu waliobobea katika eneo hilo.
Aidha, ameomba shule maalumu na za mabweni zinazohudumia wanafunzi wenye ulemavu kuwa na wasaidizi maalumu watakaowasaidia wanafunzi hao katika shughuli za kila siku ili waweze kujifunza katika mazingira bora na salama.
Katika mchango wake mwingine, Ikupa ameishauri Serikali kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa watu wenye ulemavu kwa mfumo wa ruzuku ili kuwawezesha kupata elimu kwa urahisi kutokana na mazingira wanayokabiliana nayo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha wanawake wenye ulemavu, Nassriya Nassir Ali, ameomba Serikali kujenga shule jumuishi katika kila mkoa ili kupunguza adha ya watoto wenye ulemavu kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu maalumu.
Nassriya pia ameisisitiza Serikali kuboresha miundombinu ya shule, kuongeza walimu wa elimu maalumu, kushirikisha wadau wa watu wenye ulemavu katika kuandaa sera na mitaala pamoja na kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata huduma muhimu ikiwemo bima ya afya na vifaa vya kujifunzia vinavyokidhi mahitaji yao.

Post a Comment