‎TANZANIA YAUNGA MKONO AZIMIO LA MABUNGE YA NAM-PN KULIPATIA BUNGE LA KIARABU HADHI YA MWANGALIZI. ‎

 


‎Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Daniel Sillo (Mb) amehutubia Mkutano wa 5 wa Mabunge Wanachama wa Mtandao wa Kibunge wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM-PN) na kueleza kwamba Bunge la Tanzania linaunga mkono Azimio la kulipa Bunge la Kiarabu hadhi ya mwangalizi.


‎Mhe. Sillo  ameyasema hayo leo, tarehe 15 Aprili 2026 wakati akimuwakilisha Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu kwenye Mkutano huo wa 5 wa NAM-PN uliofanyika katika Hoteli ya Hilton Istanbul

‎Bomonti, jijini Istanbul, nchini Uturuki na aliambatana na Mhe. Elibariki Kingu (Mb).


‎Katika azimio hilo, mabunge wanachama yametambua umuhimu wa msingi wa kuendeleza uhusiano na taasisi nyingine za kimataifa kama sehemu muhimu ya ujenzi wa kitaasisi na uendeshaji wenye ufanisi wa NAM-PN.

‎Aidha, azimio hilo limezingatia maombi rasmi yaliyowasilishwa na Bunge la Kiarabu ya kutaka kuwa na hadhi ya mwangalizi katika mtandao huo.



‎Kwa hatua hii, Bunge la Kiarabu sasa litashiriki vikao na shughuli za NAM-PN kama mwangalizi, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kibunge na kukuza malengo ya pamoja ya nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote.


‎Uamuzi huu uliopitishwa na Mabunge wanachana ikiwemo Tanzania, unaonesha dhamira yetu ya kujenga madaraja ya ushirikiano baina ya Tanzania na nchi za Kiarabu zilizo chini ya Bunge la Kiarabu.

Post a Comment

Previous Post Next Post