‎DKT HOMERA: MAHAKAMA YAIMARIKA KIDIJITALI




‎📌Akabidhi Kompyuta mpakato 150 kwa Mahakama.

‎📌Akabidhi Magari Matano na Kompyuta mpakato 30 kwa Tume ya haki za binadamu.


‎Na Edward Winchislaus

‎Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha sekta ya sheria nchini kwa kuwekeza katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ikiwa ni sehemu ya kuboresha utoaji wa haki kwa wananchi wote.


‎Akizungumza leo Aprili 15, 2026 katika hafla ya kukabidhi magari na vitendea kazi kwa Mahakama ya Tanzania na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, anasema serikali inalenga kuhakikisha taasisi zote zinafanya kazi kwa ufanisi zaidi kupitia mifumo ya kidijitali.


‎Amesema mafanikio yaliyopatikana katika Mahakama kwa kutumia TEHAMA yanaonyesha wazi namna teknolojia inavyorahisisha utoaji wa haki kwa wakati na kwa usahihi zaidi kwa wananchi walioko maeneo mbalimbali.

‎“Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan sikuzote inasisitiza matumizi ya TEHAMA, na tunaona mafanikio makubwa katika Mahakama namna wanavyotumia teknolojia katika utoaji wa haki,” anasema Dkt. Homera.

‎Katika hatua nyingine, wizara hiyo inakabidhi zaidi ya kompyuta mpakato  150 kwa Mahakama pamoja na magari matano na kompyuta mpakato 30 kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ili kusaidia taasisi hizo kukabiliana na changamoto za kiutendaji.

‎Hata hivyo, anakiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu duni ya TEHAMA katika baadhi ya maeneo, uelewa mdogo wa matumizi ya mifumo ya kidijitali pamoja na masuala ya usalama wa mifumo hiyo, akibainisha kuwa serikali inaendelea kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau.

‎“Niwasisitize tume na mahakama, magari haya yatunzwe vizuri kwani yamenunuliwa kwa fedha za walipa kodi, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha yanatumika kwa uangalifu,” anasisitiza.

‎Aidha, anaeleza kuwa juhudi hizo zinaendana na mkakati wa serikali wa kidijitali pamoja na dira ya maendeleo ya mwaka 2050, akisisitiza kuwa hakuna sheria itakayobaki bila kuangaliwa ili kuhakikisha inaleta maslahi mapana kwa taifa.




Post a Comment

Previous Post Next Post