Na Edward Winchislaus
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, ametembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) katika Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, ambapo amepata fursa ya kujionea maendeleo ya sekta ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi nchini.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mataragio amepata taarifa kuhusu miradi inayoendelea hususan katika maeneo ya Lindi na Mtwara, ambako shughuli za uchimbaji wa visima katika kitalu cha Mnazi Bay zinaendelea na kuonyesha mafanikio makubwa.
Akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu huyo, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau wa PURA, Bw. Charles Nyangi, amesema kazi za uchimbaji zinaendelea ambapo kisima kimoja kimeshakamilika na kingine kinaendelea kuchimbwa kikiwa kimefikia takribani mita 1,500.
Amesema, “Kwa sasa tunaendelea na uchimbaji wa visima, ambapo kisima kimoja kimekamilika na kingine kinaendelea kuchimbwa kikiwa kimefikia takribani mita 1500.”
Nyangi ameongeza kuwa kisima kilichokamilika tayari kimeanza uzalishaji wa gesi asilia na kinazalisha takribani futi za ujazo milioni 45 kwa siku kiwango ambacho kimezidi makadirio ya awali ya futi za ujazo milioni 20 kwa siku .
Baada ya kupata taarifa hizo, Dkt. Mataragio ameonesha kuridhishwa na mafanikio hayo, akisema ni ishara muhimu ya uwepo wa rasilimali kubwa ya gesi asilia nchini ambayo itaendelea kuthibitishwa kadri uchimbaji wa visima vingine unavyokamilika katika eneo hilo.
Ameipongeza PURA kwa usimamizi mzuri wa miradi ya mafuta na gesi, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji ili kuhakikisha sekta hiyo inachangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, PURA imeeleza kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi zinakuwa na tija kwa taifa na kufanyika kwa weledi wa hali ya juu.



Post a Comment