‎EWURA YALETA MAJIBU YA CHANGAMOTO ZA NISHATI BUNGENI ‎

 

‎Na Edward Winchislaus.

‎ Katika jitihada za kutatua changamoto zinazoikumba sekta ya nishati nchini, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, EWURA, imeelekeza nguvu zake Bungeni kwa kusogeza huduma, elimu na majibu ya moja kwa moja kwa wabunge wanaowakilisha wananchi.

‎Kupitia banda lake katika Wiki ya Nishati, EWURA inalenga si tu kutoa elimu, bali pia kusikiliza na kutatua hoja zinazotoka moja kwa moja kwenye maeneo ya wananchi.

‎Kaimu Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Bw. Wilfred Mwakalosi, amesema maonesho hayo ni fursa muhimu ya kuunganisha sauti za wananchi na maamuzi ya kisera.

‎“Hapa tunakutana na wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi. Tunajibu maswali yao, lakini pia tunapokea maoni yatakayosaidia kuboresha huduma za nishati,” amesema.


‎*Bei Rafiki na Ushirikishwaji wa Wananchi

‎Akielezea namna bei za huduma zinavyopangwa, Mchumi Mwandamizi kutoka idara ya udhibiti uchumi, Dkt. Achilana Mtingele, amesema EWURA huweka mizania kati ya uwezo wa mwananchi na uendelevu wa mtoa huduma.

‎Amebainisha kuwa kabla ya kupitisha bei mpya, wananchi hupewa nafasi ya kutoa maoni yao kupitia matangazo rasmi.

‎“Hatuamui bei bila ushiriki wa wananchi. Tunataka huduma ziwe nafuu lakini pia ziwe endelevu,” amesisitiza.

‎*Upatikanaji na Ubora wa Mafuta Waimarishwa

‎Kwa upande wa mafuta, Mhandisi Ibrahim Kajugusi amesema EWURA ina jukumu la kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa uhakika na kwa viwango vinavyokubalika.

‎Ameeleza kuwa mamlaka hiyo pia imerahisisha utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara ili kusogeza huduma hadi maeneo ya vijijini.

‎*Tahadhari kwa Usalama wa Umeme

‎Katika sekta ya umeme, Mhandisi Lulu Chilomba ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanatumia mafundi wenye leseni kutoka EWURA.

‎Amesema hatua hiyo itasaidia kuepuka ajali za umeme na kulinda uwekezaji wa majengo.

‎“Fundi asiye na leseni anaweza kusababisha hasara kubwa. Ni muhimu kuchagua mtaalamu aliyethibitishwa,” ameonya.

‎*Gesi Asilia Yapewa Kipaumbele

‎Nishati safi nayo imepewa uzito mkubwa, ambapo Mhandisi Evaline Rweikiza amesema matumizi ya gesi asilia yanaendelea kuongezeka, hasa katika magari na matumizi ya majumbani.

‎Amebainisha kuwa kwa sasa vituo 18 vya kujazia gesi vipo nchini, huku juhudi zikiendelea kupanua huduma hiyo nje ya Dar es Salaam ikiwemo Dodoma.

‎“Gesi asilia ni nafuu na inalinda mazingira, hivyo tunahamasisha matumizi yake kwa wananchi,” amesema.

‎Uwepo wa EWURA Bungeni umeonekana kuwa jibu la moja kwa moja kwa changamoto za nishati zinazowakabili wananchi, huku ukitoa nafasi kwa wabunge kuwasilisha kero za maeneo yao na kupata majibu ya papo kwa papo ambapo hatua hiyo inaashiria mwelekeo mpya wa uwajibikaji na ushirikishwaji katika kusimamia sekta nyeti ya nishati nchini.


‎Uwepo wa EWURA Bungeni umeonekana kuwa jibu la moja kwa moja kwa changamoto za nishati zinazowakabili wananchi, huku ukitoa nafasi kwa wabunge kuwasilisha kero za maeneo yao na kupata majibu ya papo kwa papo ambapo hatua hiyo inaashiria mwelekeo mpya wa uwajibikaji na ushirikishwaji katika kusimamia sekta nyeti ya nishati nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post