Na Edward Winchislaus
Serikali imechukua hatua kubwa kuimarisha uelewa wa Katiba na maadili nchini kwa kuingiza rasmi masomo hayo katika mitaala ya elimu kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vya ufundi stadi, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kukuza uraia mwema na utawala bora.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 24,2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa katiba na sheria Dkt.Juma Zuberi Homera wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania imefanikiwa kujumuisha maudhui ya Katiba na uraia katika mitaala ya shule za awali, msingi na sekondari, hatua inayolenga kuwajengea wanafunzi msingi imara wa uelewa wa haki na wajibu wao tangu wakiwa wadogo.
Aidha, juhudi hizo zimepanuliwa hadi elimu ya juu ambapo wizara imeandaa makubaliano na Chuo Kikuu Mzumbe ili kuanzisha rasmi ufundishaji wa somo la Katiba na maadili, likilenga kuwaandaa vijana kuwa raia wenye maadili na wanaozingatia sheria.
Katika kuimarisha elimu ya vitendo, maudhui ya Katiba na uraia pia yameandaliwa kwa ajili ya vyuo vya ufundi stadi kupitia somo la Stadi za Maisha, huku wakufunzi 26 na walimu 80 wakipatiwa mafunzo maalum ili kuhakikisha somo hilo linafundishwa kwa ufanisi katika kanda zote za VETA.
Sambamba na mageuzi ya elimu, serikali inaendelea kuboresha mfumo wa haki jinai kwa kuandaa rasimu ya Sera ya Taifa ya Haki Jinai pamoja na mkakati wake wa utekelezaji, hatua inayotarajiwa kuweka mwongozo thabiti wa kushughulikia masuala ya haki jinai nchini.
Katika kuimarisha ufanisi wa taasisi za haki jinai, wizara imeanzisha divisheni maalum ya ulinzi wa watoa taarifa za uhalifu na mashahidi, yenye lengo la kuongeza usalama, kuhamasisha ushirikiano wa wananchi, na kuhakikisha ushahidi unapatikana kwa wakati.
Teknolojia nayo imepewa kipaumbele kupitia ujenzi wa mfumo jumuishi wa TEHAMA wa haki jinai utakaowezesha taasisi mbalimbali kushirikiana kwa ufanisi zaidi, kupunguza urasimu na kuongeza uwazi katika utoaji wa haki.
Kwa upande wa utekelezaji, mafanikio yameonekana ambapo zaidi ya mashauri 166,000 yamehitimishwa mahakamani katika kipindi hicho, huku hatua za haraka za kusikiliza kesi za kiuchumi zikichangia kuachiliwa kwa trilioni 13.1 zilizoingia tena kwenye mzunguko wa uchumi, ikiashiria mchango mkubwa wa sekta ya sheria katika maendeleo ya taifa



Post a Comment