Na Edward Winchislaus,Dodoma.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua madhubuti kuboresha usafiri wa wanafunzi mijini, kufuatia kilio cha mwanafunzi kilichosambaa kupitia mitandao ya kijamii kikieleza manyanyaso wanayokumbana nayo wanafunzi wanaotumia mabasi ya mijini maarufu kama daladala.
Hatua hizo zimetangazwa leo Januari 4,2026 na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame M. Mbarawa (Mb), wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu juhudi za Serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata usafiri salama, wa uhakika na unaozingatia haki zao.
Chanzo cha hatua hizi ni barua ya mwanafunzi Mariana Eric Mirindima, wa Shule ya Sekondari Jangwani, ambaye alieleza changamoto wanazokutana nazo wanafunzi ikiwemo kugomewa kupandishwa daladala kwa madai ya kutolipa nauli kamili. Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hulazimika kusimama barabarani kwa muda mrefu, kuchelewa kufika shuleni au wakati mwingine kushindwa kabisa kuhudhuria masomo.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Prof. Mbarawa amesema hali hiyo inaathiri moja kwa moja masomo, afya ya kisaikolojia na usalama wa wanafunzi, na kusisitiza kuwa Serikali haita vumilia vitendo vinavyokiuka haki ya mtoto kupata elimu katika mazingira salama.
“Ninamshukuru mwanafunzi huyu pamoja na mzazi wake kwa ujasiri wa kutoa mrejesho. Hii ni sauti halali ya mwananchi, na nawahakikishia kuwa Serikali imesikiliza na tayari imeanza kuchukua hatua,” amesema Waziri.
Waziri amefafanua kuwa Serikali imetoa fursa kwa sekta binafsi kutoa huduma za usafiri wa umma, lakini kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za usafiri bila upendeleo.
Aidha,Katika kuboresha usafiri wa wanafunzi mijini, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha huduma za mabasi maalumu ya wanafunzi wakati wa asubuhi na jioni, kutenga mabehewa maalumu ya wanafunzi kwenye treni za mijini Dar es Salaam, pamoja na kusimamia utozaji wa nauli maalumu ya Shilingi 200 kwa wanafunzi katika daladala na mabasi yaendayo haraka.
Hata hivyo, Serikali inaendelea kutekeleza sheria ya kuthibitisha madereva na kusajili makondakta wa vyombo vya usafiri wa umma, hatua inayolenga kuimarisha nidhamu, usalama na staha ya huduma.
Ili kuhakikisha utekelezaji wa hatua hizo, Waziri Mbarawa ameielekeza LATRA kuimarisha ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kutoa adhabu kali kwa madereva na makondakta watakaobainika kuwanyanyasa wanafunzi, pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa watoa huduma na abiria kuhusu haki na wajibu wao.


Post a Comment