BILIONI 5 KUZIWEZESHA KAMPUNI CHANGA ZA TEHAMA;WAZIRI KAIRUKI ‎

 


‎Na Edward Winchislaus,Dodoma

‎Serikali imesema utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari umeleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, hususan katika upatikanaji wa mawasiliano, huduma za kidijitali na fursa za kiuchumi.

‎Akizungumza na waandishi wa habari Februari 4, 2026, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah  Kairuki, amesema Serikali imejikita kuhakikisha TEHAMA inatumika kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida mijini na vijijini.

‎Pia,waziri Kairuki amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuwezesha kampuni changa za TEHAMA, hatua itakayowezesha vijana kujiajiri, kuajiri wengine na kutoa huduma bunifu katika sekta za afya, elimu, kilimo, fedha na biashara.

‎Katika kuongeza uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi, Wizara imeunganisha taasisi 800 za umma kwenye Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali (GovNet), hali inayowawezesha wananchi kuwasilisha kero zao kwa njia ya kidijitali na kupata majibu kwa wakati.

‎Aidha,upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano umeendelea kuboresha maisha ya wananchi vijijini baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano katika kata 713, hatua iliyoongeza upatikanaji wa huduma za simu, intaneti na huduma za kifedha kwa njia ya simu.


‎Hata hivyo,serikali imeendelea kudhibiti gharama za mawasiliano ambapo bei ya kupiga simu ndani ya nchi imeendelea kubaki shilingi 29 kwa dakika, jambo linalowawezesha wananchi wengi kumudu huduma hizo.


‎Katika kuimarisha upatikanaji wa taarifa na huduma za Serikali, Wizara imepeleka huduma ya Wi-Fi katika maeneo ya umma ikiwemo masoko, hospitali, stendi za mabasi na vyuo, hatua inayoongeza matumizi ya intaneti miongoni mwa wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post