SIKU 100 ZA SERIKALI YA AWAMU YA SITA:VIWANDA,AJIRA NA FURSA MPYA KWA VIJANA

 

‎Na Edward Winchislaus,Dodoma.

‎Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha mwelekeo mpya wa kujenga uchumi wa viwanda unaozalisha ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kuiweka Tanzania katika ramani ya biashara ya kikanda na kimataifa.

‎Akizungumza na waandishi wa habari,januari 24,2026 jijini Dodoma Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Judith Kapinga amesema kuwa katika siku 100 tangu Uchaguzi Mkuu, sekta ya viwanda na biashara imepata mafanikio makubwa yanayopimika, hususan katika uwezeshaji wa wajasiriamali, vijana na uwekezaji wa viwanda.

‎Kwa mujibu wa Waziri huyo, zaidi ya mikopo 193 yenye thamani ya shilingi milioni 821.7 imetolewa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kupitia SIDO katika mikoa 19 nchini, hatua iliyozalisha ajira 546, kati ya hizo 436 zikiwa za vijana.

‎Pia ameeleza kuwa Serikali imeweka mkazo katika kupeleka viwanda karibu na wananchi kupitia mitaa ya viwanda na kongani, ambapo tathmini imefanyika katika mikoa 11, huku maeneo manne ya SIDO yakiwa tayari kwa uzinduzi rasmi mwezi Februari 2026.

‎Katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, viwanda vidogo vya kuchakata alizeti, muhogo, mafuta ya kula na nishati mbadala vimeanza uzalishaji, vikitarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 1,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hasa kwa vijana na wanawake.

‎Sekta ya uwekezaji mkubwa nayo imepata msukumo mpya baada ya wawekezaji wakubwa kuanza kuwekeza katika Kongani ya TAMCO, ikiwemo miradi ya kuunganisha magari ya mafuta na ya umeme, pamoja na viwanda vya chakula cha mifugo.

‎Aidha, kupitia BRELA, Serikali imesajili zaidi ya kampuni 4,200 na majina ya biashara 7,498, ambapo asilimia kubwa ni za vijana, hatua inayochochea urasimishaji wa biashara na ukuaji wa ajira rasmi.

‎Kwa upande wa masoko, TanTrade imeimarisha mifumo ya kidigitali ya taarifa za biashara, huku zaidi ya wafanyabiashara 26,000 wakipata taarifa za masoko ya ndani na nje ya nchi.

‎Katika mazao ya kimkakati, mfumo wa stakabadhi za ghala umehakikisha zaidi ya shilingi trilioni moja zinaingia mikononi mwa wakulima wa korosho msimu wa 2025/2026, hatua iliyoboreshwa kipato cha wakulima na mapato ya Halmashauri.


‎Waziri amesema mafanikio haya ni ishara ya mwanzo wa safari ya kujenga uchumi wa viwanda, uchumi wa ubunifu na uchumi wa kijani, akiwahimiza vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika viwanda vidogo, biashara na masoko ya kimataifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post