Na Edward Winchislaus,Dodoma.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepata mafanikio makubwa katika zoezi la utambuzi, urasimishaji na uwezeshaji wa wafanyabiashara ndogondogo na wajasiriamali wa sekta isiyo rasmi ndani ya siku 100 za mwanzo wa kipindi cha pili cha uongozi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 25,2026 jijini Dodoma Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe.Dorothy Gwajima amesema sekta isiyo rasmi imeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa kwa kuwaajiri mamilioni ya Watanzania hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Amesema kuwa kwa muda mrefu sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kutokutambulika kisheria, ukosefu wa mitaji na masoko pamoja na kukosa ulinzi wa kijamii, hali iliyosababisha Serikali kuweka mkazo mkubwa katika urasimishaji wake kama mkakati wa kujenga uchumi jumuishi.
Katika kipindi cha siku 100, Wizara imesajili jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 119,595 kupitia Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Wafanyabiashara Ndogondogo ambapo wanawake ni 73,341 na wanaume 46,254. Kati yao, machinga ni 103,102, mama na baba lishe 12,384 na waendesha bodaboda na bajaji 4,109.
Aidha, Serikali imetoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia saba kwa mwaka kupitia Benki ya NMB, ambapo Shilingi bilioni 1.35 tayari zimetolewa kwa wafanyabiashara 588, huku Shilingi bilioni 10.5 zikitengwa kwa ajili ya zoezi hilo nchi nzima. Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, wanawake wajasiriamali 45 wamepatiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 337.9 kwa riba ya asilimia nne.
Kwa upande wa urasimishaji wa usafiri, waendesha pikipiki na bajaji 209,632 wamerasimishwa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kupatiwa leseni za udereva, hatua inayowawezesha kufanya kazi zao kwa usalama na uhalali wa kisheria.
Serikali pia imewafungulia wajasiriamali masoko ya uhakika kwa kuwarasimisha katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST), ambapo vikundi 1,123 vya makundi maalum vimepata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 31 kupitia fursa ya asilimia 30 ya manunuzi ya umma.
Hata hivyo Waziri Gwajima amewahimiza wafanyabiashara ndogondogo na wajasiriamali kuendelea kujitokeza kwa wingi kujisajili kwenye mifumo ya Serikali ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa, akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika safari ya maendeleo.





Post a Comment