Na Edward Winchislaus, Dodoma
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Fadhili Maganya, amesema mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yana mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana nchini.
Akizungumza Januari 17, 2026, wakati wa ziara ya viongozi wa Umoja wa Wazazi wa Tanzania katika Makao Makuu ya VETA jijini Dodoma, Maganya amesema kuwa mafunzo hayo yanaendelea kutoa mwelekeo mpya kwa vijana na kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Pia,amesisitiza kuwa wazazi na walezi wana jukumu la msingi katika kuwaelekeza vijana kuchagua mafunzo ya ufundi stadi, pamoja na kuwajengea ujasiri wa kujiajiri kupitia ujuzi watakaoupata.
Aidha,Maganya ametoa rai kwa jamii kubadili mtazamo hasi uliokuwepo dhidi ya elimu ya ufundi, akieleza kuwa mafunzo yanayotolewa na VETA ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa na msingi wa upatikanaji wa ajira.
Ameongeza kuwa kozi mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo zinawawezesha vijana kujiajiri mara baada ya kuhitimu, huku akieleza kuwa tatizo la ajira ni la kimataifa na Tanzania haipo tofauti sana na mataifa mengine.
Kwa mujibu wake, wahitimu wa VETA wamekuwa wakipewa nafasi kubwa katika soko la ajira kutokana na ujuzi walioupata, na kwamba CCM inaendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha ajira kwa vijana kupitia elimu ya ufundi.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Omar, kwa niaba ya Waziri Prof. Adolf Mkenda, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonesha dhamira thabiti ya kuhakikisha vijana wanapata ajira kupitia elimu yenye kuzingatia ujuzi.
Dkt. Omar amesema serikali imefanya maboresho katika sera ya elimu kwa kuongeza msisitizo kwenye elimu ya ufundi na ujuzi, hatua inayolenga kuwaandaa vijana kuajiriwa au kujiajiri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema mamlaka hiyo imeendelea kupanua wigo wa mafunzo kwa kuongeza vyuo zaidi ya 30 katika maeneo mbalimbali nchini, na kufikisha jumla ya vyuo 80, huku vyuo 65 vikiwa katika hatua tofauti za ujenzi.
Kasore amesema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na VETA imeongezeka kutoka 61,000 hadi kufikia 86,000 kwa mwaka, kwa kozi za muda mfupi na mrefu, ambapo serikali imeendelea kugharamia kwa kiasi kikubwa ada za masomo.
Ameeleza kuwa serikali imetenga takribani shilingi bilioni 7.2 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kujifunzia katika vyuo vya zamani, ili kuendana na maendeleo ya teknolojia, na zaidi ya vyuo 60 vimenufaika na mpango huo.
Kasore ameongeza kuwa idadi ya wasichana wanaojiunga na mafunzo ya ufundi imeongezeka kutoka asilimia 20 hadi 30, hali inayoonesha kuimarika kwa mwamko wa jamii kuhusu elimu ya ufundi.
Aidha, amesema VETA inaendesha mpango wa kurasimisha ujuzi kwa watu wenye ujuzi walioupata nje ya mfumo rasmi wa elimu, ambapo vijana zaidi ya 22,000 tayari wameshapatiwa vyeti.
Amebainisha kuwa lengo la mamlaka hiyo ni kuwafikia vijana 100,000 kote nchini ili kuhakikisha kila mkoa unapata manufaa ya mpango huo.





Post a Comment