CCM KUANZA ZIARA YA KITAIFA KUSIKILIZA, KUTATUA KERO ZA WANANCHI SINGIDA

 


‎Na Edward Winchislaus.

‎Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi, amesema chama hicho kinatarajia kuanza ziara ya kikazi na kimkakati nchi nzima kuanzia Januari 19, 2026, ikiwa na lengo la kukagua utekelezaji wa ahadi za kampeni, kuimarisha chama na kusikiliza kero za wananchi.

‎Akizungumza na waandishi wa habari leo januari 17.2026 jijini Dodoma, Kihongosi amesema ziara hiyo itaanzia Mkoa wa Singida, ambapo msafara utaanza katika Wilaya ya Manyoni kabla ya kutembelea wilaya zote za mkoa huo hadi Januari 22, 2026.

‎Amesema ziara hiyo ni sehemu ya dhamira ya CCM kushuka chini kukutana ana kwa ana na wananchi, wapenzi, mashabiki na wanachama wa chama hicho ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.

‎“Tunakwenda kuangalia yaliyoahidiwa wakati wa kampeni kama yametekelezwa, kama yako kwenye mchakato wa utekelezaji au kama yapo kwenye mipango ya kutekelezwa. Zipo ahadi ambazo zimetekelezwa kwa asilimia 100, nyingine zinaendelea, na nyingine zitakamilika kabla ya siku 100 kutimia,” amesema Kihongosi.

‎Ameongeza kuwa ziara hiyo pia italenga kuendelea kukijenga chama, kuhamasisha wanachama na wananchi kusimama imara kukilinda chama chao, serikali na taifa kwa ujumla, sambamba na kuchochea amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.

‎“Chama Cha Mapinduzi kipo imara na kinaendelea kusonga mbele. CCM haijengwi kwa maneno, inajengwa kwa vitendo. Siasa ya nchi yetu inaendelea kukua na kukubalika ndani na nje ya nchi, hali inayochangia mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali,” amesema.

‎Katika ziara hiyo, Kihongosi amesema viongozi wa chama watashuka hadi ngazi ya mashina na kukutana na mabalozi wa CCM, akisisitiza kuwa ziara hiyo itakuwa ya kipekee. Aidha, aliwataka viongozi wa umma katika maeneo yatakayopita msafara huo kuhakikisha wanakuwepo ili kujibu kero zitakazowasilishwa na wananchi.

‎Katika hatua nyingine, Kihongosi alitoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mkutano wake na mabalozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali uliofanyika Januari 15, 2026, akisema chama kimeridhishwa na kufurahishwa na mkutano huo wa ufunguzi wa mwaka.

‎“Tunaipongeza kwa dhati Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha uhusiano mwema wa kidiplomasia na kulinda hadhi ya nchi yetu kimataifa,” amesema.

‎Ziara hiyo ya CCM inatarajiwa kuendelea katika mikoa mingine baada ya kukamilika kwa ratiba ya Mkoa wa Singida, huku chama kikiendelea kusisitiza siasa za kusikiliza wananchi na kutatua changamoto zao kwa vitendo.

Post a Comment

Previous Post Next Post