Na Edward Winchislaus
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekabidhi pikipiki 36, magari 33 na droni tatu kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usimamizi wa misitu ya taifa.
Vitendea kazi hivyo vimenunuliwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3.25 na vinatarajiwa kuongeza ufanisi wa askari wa uhifadhi katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan yale yenye changamoto za miundombinu na kufikika.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo leo Desemba 30, 2025 jijini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amesema serikali imeendelea kuwekeza katika vitendea kazi kwa kutambua umuhimu wa kulinda rasilimali za taifa, ikiwemo misitu na maeneo ya hifadhi.
“Mnajua kuwa Tanzania imehifadhi takribani theluthi moja ya eneo lote la nchi yetu kwa ajili ya hifadhi za taifa, misitu na mapori mbalimbali. Ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi zetu, serikali imeendelea kununua vitendea kazi,” amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, amesema jukumu kubwa la TFS ni kuanzisha, kutunza na kuhifadhi misitu ya asili iliyopo, akibainisha kuwa wakala huo umeendelea kuanzisha misitu mipya na kutunza ile iliyopo katika halmashauri mbalimbali kwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa.
Ameongeza kuwa TFS ina kanda saba nchini, na vitendea kazi hivyo vitasambazwa katika kanda zote ili kuhakikisha huduma za uhifadhi zinafika kwa wananchi walipo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania, Profesa Dos Santos Silayo, amesema vifaa hivyo vitawawezesha askari wa uhifadhi kukabiliana na changamoto za uhifadhi kwa ufanisi zaidi kupitia matumizi ya nyenzo na teknolojia za kisasa.
Prof. Silayo amesema TFS imewekeza katika matumizi ya teknolojia ya setilaiti na droni ili kupata taarifa za haraka kuhusu matukio ya moto na uharibifu wa misitu.
“Tunatumia ndege nyuki (droni) ambazo zinatupa taarifa kwa wakati kulingana na maeneo tunayoyahitaji, jambo linalotuwezesha kuchukua hatua za mapema,” amesema.
Naye Askari wa Uhifadhi Daraja la Kwanza (CR1), Ally Msuya, amesema droni hizo zimekuwa msaada mkubwa katika kubaini maeneo yenye moto, hususan katika milima na mabonde ambako kufika kwa urahisi ni changamoto.
“Droni hizi zina uwezo wa kufika umbali wa kilomita 20 na kupaa hadi mita 5,000 kutoka ardhini. Zimetumika kwa mafanikio katika kudhibiti moto Mlima Hanang,” amesema Msuya.
Kukabidhiwa kwa vitendea kazi hivyo kunaonesha dhamira ya serikali ya kuimarisha uhifadhi wa misitu kwa kutumia teknolojia na nyenzo za kisasa, hatua inayolenga kulinda rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Post a Comment