Na Edward Winchislaus
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imewatahadharisha wadaiwa wa viwanja katika maeneo ya Mtumba na Kikombo kuhakikisha wanalipa madeni yao ndani ya siku 21 kuanzia sasa, la sivyo viwanja hivyo vitachukuliwa na kurejeshwa sokoni.
Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 29, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Bw. Denis Harrison Gondwe, wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini hapa.
Bw. Gondwe amesema kuwa iwapo Taasisi, kampuni au mtu binafsi atashindwa kulipa ndani ya muda uliopangwa, Halmashauri hiyo haitasita kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kurudisha viwanja hivyo na kuviuza upya.
"Wito kwa wote wanaodaiwa Mtumba zone 2,Mtumba zone 3 na Kikombo wajitokeze kukamilisha malipo ya viwanja hivyo ndani ya siku 21,"amesisitiza.
Amesisitiza kuwa malipo hayo ni muhimu ili kuwezesha utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo ya Halmashauri, kwani mapato yatokanayo na viwanja hivyo tayari yamejumuishwa kwenye bajeti ya Halmashauri ya Jiji.
Kwa mujibu wa Bw. Gondwe, jumla ya thamani ya viwanja ambavyo bado havijalipiwa ni shilingi bilioni 55.4. Kati ya hivyo, wadaiwa wa Mtumba Zone 2 wanadaiwa shilingi bilioni 28.8, Mtumba Zone 3 shilingi bilioni 20.6, huku eneo la Kikombo likiwa na deni la shilingi bilioni 5.9.
Katika hatua nyingine, Bw. Gondwe amewataka watu binafsi, taasisi au kampuni zilizokamilisha malipo hayo lakini majina yao yanaonekana kwenye orodha ya wadaiwa, kufika katika ofisi za Halmashauri hiyo wakiwa na nyaraka halali za malipo kwa ajili ya uhakiki na marekebisho.

Post a Comment