WANAWAKE DODOMA WAIMARISHA UWEZESHAJI KIUCHUMI KUPITIA MAJUKWAA YA MAENDELEO



‎Na Edward Winchislaus.

Wanawake wa Jiji la Dodoma wameendelea kunufaika na Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, ambayo yamekuwa chachu ya mabadiliko katika maisha yao na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi katika jamii. Hayo yamebainishwa Novemba 28, 2025 wakati Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi MaryPrisca Mahundi alipokutana na viongozi na wajumbe wa jukwaa hilo.

‎Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri MaryPrisca alisema majukwaa hayo yameongeza uelewa wa wanawake kuhusu masuala ya fedha, kuwawezesha kijumla kiungozi na kuwapa ujasiri wa kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi. 

‎“Majukwaa haya ya wanawake yana umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya wanawake na yameanzishwa ili kutoa fursa kwa wanawake kuweza kukutana, kuchochea ubunifu na ushirikiano, kupitia mafunzo, midahalo na kubadilishana uzoefu kati ya wanawake wa maeneo mbalimbali,” alisema.

‎Alifafanua kuwa kupitia majukwaa hayo, wanawake wanajengeana uwezo katika nyanja nyingine za maisha ikiwemo kuendeleza Tunu za Taifa, Uraia, uzalendo na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, hatua inayosaidia kujenga jamii salama na yenye mshikamano.

‎Hata hivyo, Naibu Waziri alikiri kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha majukwaa hayo yanazidi kuwa na tija zaidi,ambapo amehimiza kuongeza ushirikiano baina ya sekta binafsi, taasisi za kifedha, Serikali na wadau mbalimbali ili kuwawezesha wanawake kupata elimu ya kibiashara, fursa za masoko, teknolojia bora na mitaji rafiki inayowasaidia kupiga hatua katika shughuli zao.

‎Amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu ili kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha wanawake katika kupata mikopo, hivyo kuchochea ushiriki wao katika kukuza uchumi wa Taifa. “Napenda kuwahakikishia kuwa jitihada hizi za kuwezesha majukwaa si tu zinawanufaisha wanawake peke yao, bali zinaimarisha familia, jamii na Uchumi wa Taifa kwa ujumla,” alisema Naibu Waziri MaryPrisca.

‎Katika hatua nyingine, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Dodoma imeahidi kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Jukwaa la Viongozi la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Jiji la Dodoma ili kuhakikisha mazingira wezeshi ya biashara yanaimarishwa. Hatua hii inalenga utekelezaji wa sera na miongozo rafiki na kuwatengenezea wanawake fursa zaidi za kimaendeleo bila ubaguzi.

‎Mkutano huo umeonesha kuwa uwezeshaji wa wanawake kupitia majukwaa unaendelea kuleta mabadiliko makubwa katika ngazi ya jamii, huku wanawake wa Dodoma wakionekana kuwa mfano wa mafanikio ya juhudi za kujitegemea. Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha juhudi hizo ili kukuza uchumi shindani na jumuishi.

‎Hatua hizi kwa pamoja zimetajwa kuwa msingi muhimu wa maendeleo ya kitaifa, kwani kama alivyosisitiza Naibu Waziri, “Jitihada za kuwainua wanawake ni jitihada za kulijenga Taifa; wanawake wanapowezeshwa, Taifa .”

Post a Comment

Previous Post Next Post