Na Edward Winchislaus.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Mhe. Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa katika kipindi hiki cha mageuzi ya teknolojia, ni muhimu elimu ichukue nafasi ya kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto pamoja na kutumia fursa za utandawazi ambao sasa umegeuka kuwa dira na mwelekeo wa dunia nzima.
Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo leo Novemba 27, 2025 jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa walimu wakuu wa shule za msingi Tanzania Bara (TAPSHA). Amesema utandawazi ni fursa kubwa kwa mataifa yaliyojiandaa, lakini pia huibua changamoto zinazohitaji mfumo madhubuti wa elimu unaomuwezesha kijana kuibuka na kutumia kikamilifu fursa hizo.
“Mageuzi ya elimu faida yake ni kwa kizazi kijacho. Mwana siasa mwepesi atakwepa hilo na kutafuta yale malaini laini. Mageuzi ya elimu yanahitaji uvumilivu, siyo suala la dharura, na hilo ametuonesha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Amefafanua kuwa mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani yanabadilisha mfumo wa uzalishaji na utoaji huduma kwa kasi, hatua inayoongeza tija katika uchumi wa mataifa mbalimbali. Ametoa angalizo kuwa endapo Tanzania haitajiandaa kupitia elimu, hususan Sayansi na Teknolojia, itaendelea kubaki mnunuzi wa bidhaa kutoka nje.
“Rais wetu alisema sababu nyingine ya mageuzi ya elimu ni mfumko huu mkubwa wa Sayansi na Teknolojia duniani unaorahisisha utoaji wa huduma, uzalishaji wa bidhaa na hata kupunguza bei zake. Lakini kama sisi hatutaweza kwenda kwa kasi hiyo, hatutaweza kuzalisha bidhaa kwa bei nafuu. Hapo ndipo utandawazi utakuja kutugonga tena na vijana wetu wengi watakosa ajira,” amesema.
Aidha, Waziri Mkenda amesema halmashauri zote nchini zinapaswa kubainisha maeneo yatakayoongezewa madarasa ya sekondari ili kupunguza umbali unaowalazimu wanafunzi kutembea kwenda shule za ngazi hiyo.
Katika hatua nyingine Profesa Mkenda amewataka walimu nchi nzima kutoa tathmini ya utekelezaji wa mtaala mpya kwa kuzingatia kile wanachokiona wanapotekeleza majukumu yao ya ufundishaji darasani. Ameeleza kuwa ni muhimu walimu kubainisha changamoto zilizopo kwenye mtaala mpya pamoja na maeneo mazuri yanayohitaji kuboreshwa zaidi, kwa kuwa suala la mtaala ni endelevu na hutegemea mrejesho wa watendaji wa moja kwa moja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAPSHA, Bi. Rehema Ramole, amemuomba Waziri kuhakikisha wakuu wa shule wanapatiwa mafunzo ya kutosha kuhusu mitaala iliyoboreshwa, sambamba na kushirikishwa kikamilifu katika tathmini za mabadiliko hayo.
Amesema lengo la TAPSHA ni kuwaunganisha wakuu wa shule za msingi nchini ili kushirikiana kutatua changamoto za kitaaluma, na kuwawezesha wanachama kupitia semina za uongozi na mikutano inayolenga kuboresha uwezo wao wa kiutawala.

Post a Comment