MAJALIWA AAGIZA MAMBO 3 WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI JUU YA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI ULIYOZINDULIWA

 



Na Edward Winchislaus .

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( Mb)  Mhe.Kassimu Majaliwa  ameiagiza Wizara ya mawasiliano na Teknolojia ya Habari kukamilisha maandalizi ya sheria ya anwani za makazi ili kuweka masharti ya msingi katika utumiaji wa anwani hizo katika utoaji na upokeaji wa  huduma pamoja na kuhakikisha maadhimisho ya anwani ya makazi yanakuwa endelevu kila mwaka.



Maagizo hayo ameyatoa leo Februari 8,2025 wakati wa kilele cha Maadhimisho ya wiki ya anwani ya makazi yaliyofanyika Jijini hapa Dodoma yakiambatana na kauli mbiu isemayo tambua na tumia anwani ya makazi kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma.


"kama mnavyofahamu suala la anwani za makazi ni moja ya mambo yaliyopewa kipaumbele katika mpango wa miaka mitano ya maendeleo ya Taifa letu uliyoanza mwaka wa Fedha 2021/2022 na unakwenda mpaka mwaka huu 2025/26 na mpango huu umeweka bayana adhima ya serikali ya kujenga mfumo wa anwani za makazi katika kata zote hapa nchini na mpango huu unatekelezwa ukiwa sambamba na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.


"Naomba nisisitize mambo muhimu ambayo tunapaswa tuyazimgatie kwa watendaji wetu,kwa Wizara ya mawasiliano na Teknolojia ya habari kamilisheni maandalizi ya sheria ya anwani na makazi,pili hakikisheni kwamba maadhimisho haya yanakuwa endelevu yameanza mwaka huu yasiishiye mwaka huu kwasababu tumeona matunda yake,Tatu,endeleeni kushirikiana na wadau ambao wanajihusisha na mambo ya kidijitali  mratibu upatikani wa vifaa mbalimbali ili kuhakikisha mfumo huu unafanikiwa",amesema Majaliwa.


Pia amesema kuwa mfumo huo unazofaida mbalimbali ikiwa ni pamoja na  kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii kwenye maeneo ya kila mmoja pamoja na uboreshaji wa ulinzi na usalama nchini kwa kutambua eneo la tukio lilipo tokea.



vilevile mfumo huo umeelezwa kuwa utachochea uchumi nchini ikiwa ni pamoja na kuwezesha biashara ya mtandaoni.


"Siku kama ya leo tarehe 8 mwezi wa pili mwaka 2022 Rais wetu  Mhe.Dkt samia Suluhu Hassan alizindua utekelesaji wa anwani za makazi hapa nchini kwa njia ya oparesheni,opareshini hiyo ilifanyika kwa miezi minne na ikawezesha kukusanya taarifa zaidi ya milioni 12.3 za anwani ya makazi  kote nchini na kuwezesha mamlaka za mitaa kutambua barabara na mitaa na kuweka majina ya mitaa pamoja na namba za nyumba zetu na kutambua idadi ya nyumba zote nchini",amesema.



Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya habari Mhe.Jerry Slaa ameeleza kuwa Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ulianza mwaka 2010 na kwa mujibu wa Mpango wa utekelezaji ulitakiwa ukamilike mwaka 2015 ambapo  mwaka 2015 utekelezaji ulifikia asilimia mbili na kushindwa kukamilika kama ilivyopangwa kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za ufinyu wa fedha.


Pia ameongeza kuwa  wiki hii shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo kutoa elimu kwa umma kuhusu mfumo wa anwani za makazi ambapo imetolewa kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii pamoja na kutembelea maeneo yenye mikusanyiko kama Stendi za mabasi, Vituo vya pikipiki (maarufu kama bodaboda) kukutana na wafanyabiashara wadogo wadogo sambamba na mafunzo maalum kwa wanachuo wa baadhi ya Vyuo vilivyopo Dodoma kuhusu mfumo wa anwani za Makazi. 


"Mfumo haukukamilika kutokana na ugumu wa utekelezaji wa Mfumo kwa kukosekana kwa jitihada za pamoja miongoni mwa wadau wa utekelezaji hata hivyo ilipofika Januari, 2022, utekelezaji ulifikia asilimia tatu hali ambayo bado kasi ya utekeleza ilikuwa siyo ya kuridhisha Katika kukabiliana na changamoto hizo na kwa kuzingatia manufaa ya mfumo kijamii na kiuchumi ukiwemo uchumi wa kidijitali",Ameeleza.


Katika hatua nyingine Silaa amesema kuwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kusimamia na kuendeleza miundombinu na mifumo ya msingi (Foundation Systems), ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa kidijitali ulioainishwa katika Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Miaka 10 (2024/2034),Mifumo hii inajumuisha mifumo ya utambuzi wa watu, biashara, ardhi, na makazi.

Post a Comment

Previous Post Next Post