MEI MOSI :SUALA LA ONGEZEKO LA MSHAHARA WAFANYAKAZI WATAKIWA KUWA NASUBIRA MAMA ATASEMA JAMBO

 Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza awaambie Wafanyakazi wa Tanzania kuwa endapo hali ya uchumi wa Taifa itaendelea kuwa stahimilivu na kudumu kama ilivyo sasa basi Wafanyakazi wawe na matumaini kwamba atasema jambo hivi karibuni kuhusu nyongeza ya mishahara.



Akiongea leo wakati wa Maadhimisho ya Mei Mosi, Dkt. Mpango amesema “Kuhusu nyongeza ya mishahara kama mlivyosema kwenye risala yenu mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilipandisha kima cha chini cha mishahara kwa 23.3% kutoka Tsh. 300,000 hadi Tsh. 370,000 kwa mwezi lengo likiwa ni kuwezesha Watumishi wenye mishahara ya kima cha chini kumudu gharama za maisha kadri inavyowezekana” 


“Makundi mengine ya Watumishi nayo yaliguswa na ongezeko hilo la mishahara kwa viwango tofauti kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya mishahara iliyotengwa,  kama ambavyo tumekuwa tukisema Serikali itaendelea kuhuisha viwango vya mishahara kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi na kibajeti pamoja na ujuzi na utendaji wa Waajiriwa, haya ni muhimu ili kuepuka kuchochea mfumuko wa bei, kuhatarisha uhimilivu wa deni la Taifa na athari nyingine kwenye utulivu wa uchumi wa Taifa kwa ujumla”


“Haya yote lazima yazingatiwe katika mchakato wa  kuongeza mshahara hususani katika kipindi ambapo uchumi wa Dunia umekumbwa na misukosuko mingi ikiwemo Vita za Urusi na Ukraine na vita vya Mashariki ya Kati inayohusisha Palestina, Israel, Lebanon, Syria na Iran na kufanya kuvurugika kwa bei ya ugavi na kupanda sana kwa bei ya chakula ,mbolea, mafuta n.k”


“Kama hiyo haitoshi Dunia imekumbwa na majanga mengine ikiwemo mvua kubwa na maporomoko ya ardhi ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, magonjwa na hata vifo, changamoto zote hizi zimeathiri uchumi wetu lakini bado pamoja na haya yote tathmini tulizofanya ndani na zilizofanywa na IMF, Benki ya Dunia n.k zimeonesha uchumi wa Taifa umekuwa stahimilivu kwa kiasi cha kuridhisha na Nchi yetu inakopesheka” 


“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mama wa Taifa ameniagiza niwaambie Wafanyakazi wa Tanzania kuwa endapo hali hiyo itadumu Wafanyakazi wawe na matumaini kwamba atasema jambo hivi karibuni“ 


Post a Comment

Previous Post Next Post