Na Paul Kayanda, Kahama
SHIRIKA la Kutetea Haki za Binadamu katika Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga(SHIHABI) limeingilia kati mgogoro wa shamba lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 90 baina ya Mwananchi Jonathan Miyekello aliyeulalamikia uongozi wa Kijiji cha Ngokolo Kata ya Bukomela Halmashauri ya Ushetu kupokonya mashamba yake na kuweka mabango ya onyo kwa madai ni makubaliano ya Kijiji na wananchi kupisha Mradi wa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Miyekello amefikisha malalamiko yake katika ofisi za Shirika hilo akilalamikia uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Ngokolo kwamba imevamia mashamba yake na kuweka mabango ya onyo juu ya matumizi ya mashamba hayo kutokana na makubaliano ya mkutano mkuu wa Kijiji hicho ili kupisha Mradi wa mpango wa matumizi bora ya ardhi unaotarajiwa kuja kunufaisha wanakijiji.
Aidha akiwa katika Ofisi hizo mwanakijiji huyo amelalamika kuwa jumla ya mashamba yake mawili yenye zaidi ya ekari 90 yamesimikwa mabango yanayokataza matumizi ya shughuli zozote kuendelea ndani ya eneo hilo ili kupisha mradi wa mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi unaodaiwa kutamburishwa kwa wanakijiji cha Ngokolo.
“Kwenye mkutano mkuu wa kijiji wa kutambulishwa Mradi wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi tuliambiwa tutamilikishwa mashamba yetu kimila kwanza lakini kabla ya kumilikishwa tumeshangaa kuona mabango yenye onyo kali la kutotumia maeneo yetu yamesimikwa kwenye mashamba yetu na tukiuliza hiki kimefanyika kwa kikao gani na muhutasari gani hatupewi majini na kijiji,” amelalamika Miyekello.
Aidha anatumia nafasi ya kukutana na Shirika hilo kuiomba Serikaliiwamilikishe kwanza wananchi maeneo ya mashamba yao kama walivyoahidiwa katika mkutano huo mkuu kwa kuwa hakuna muhutasari wowote wa makubaliano ya kusimika mabango ulioridhiwa na wananchi.
“Mkurugenzi wa Halmashauri anapaswa kufika kwenye maeneo yetu atufafanulie yeye mwenyewe kama ametupokonya mashamba yetu, maana huu ni ujanja wa viongozi wa kijiji pamoja na mwenyekiti wao ili watupokonye maeneo yetu wauze,” anasema kwa uchungu mwananchi huyo.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ngokolo Masalu Mayenga amekili Mabango hayo kusimikwa ndani ya maeneo ya mashamba ya wananchi ni kufuatia makubaliano ya mkutano mkuu wa kijiji kuwa maeneo hayo yanatwaliwa na Serikali ili yatumike kwa mradi wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kwa maslahi ya Umma.
Kufuatia hali hiyo Mayenga amesema kuwa atahakikisha kuwa anatekeleza maagizo ya Ofisi hiyo ya kuondoa mabango hayo kwenye mashamba ya wananchi wa Kijiji cha Ngokolo mpaka hapo utaratibu utakapofuatwa.
Kwa upande wake kaimu mwenyekiti wa Shirika hilo Solomon Juma Kitigwa ameiagiza Serikali ya kijiji hicho kuondoa mabango hayo yaliyosimikwa kinyume na utaratibu wa matakwa ya Mradi huo.
Amesema kuwa pamoja na Ardhi ni mali ya Serikali kunautaratibu wa kufuata pale serikali inapohitaji Ardhi yake ambayo tayari inakuwa na mmiliki wake na kuongeza kuwa ili kuepusha usumbufu kwa wananchi Serikali hiyo ya kijiji ifuate taratibu zote za kutwaa maeneo ya wananchi.
“Shirika limefnya jitihada za kumsaidia na kufauru kumkutanisha na Ofisa Mtendaji wa Kijiji na pia mwenyekiti wa Kijiji cha Ngokolo na kujadiliana nao kwa kina,” amesema Kitigwa kaimu mwenyekiti SHIHABI.
Pamoja na mambo mengine katika kikao hicho amesema kwa pamoja wamekubaliana pande zote kuwa mabango yaliyowekwa ndani ya mashamba ya ndugu Jonathan John Miyekello yatolewe mara moja ili kusubili taratibu za Mradi huo.



Post a Comment