Na Mwandishi wetu- Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema anaandaa utaratibu mzuri wa kushirikiana kwa karibu na waongoza utalii wa Mikoa ya Rukwa na Katavi kwa lengo la kujua kazi zao, changamoto zao na kupata maoni ili kufungua utalii wa mikoa hiyo.
Ameyasema hayo leo katika kikao kati yake na Wabunge wa Mikoa ya Rukwa na Katavi kilichofanyika ukumbi wa Utawala Bungeni jijini Dodoma leo.
Amesema ameshafanya utafiti kujua waongoza utalii walioko katika mikoa hiyo na kupata mawasiliano yao na ataanza kuunda kundi sogozi (whatsapp) ili kuwasiliana nao zaidi kutatua changamoto zao.
Amefafanua kuwa mpaka sasa waongoza watalii hao wamewasilisha baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo katika kazi zao ikiwa ni pamoja na bei ya ndege za watalii na kufafanua kwamba atakaa na Waziri wa Sekta ya Uchukuzi kuona ni namna gani wanashughulikia changamoto hiyo.
Pia amesema wameongelea changamoto ya miundombinu ya barabara kuelekea maeneo ya hifadhi akitolea mfano wa barabara ya Katavi kwenda Mahale, Ifukutwa-Rukoma kupitia Mwese ambazo ameahidi kuangalia namna ya kuziboresha kwa kushirikiana na Sekta husika.
Ameweka bayana kuwa, Serikali inaangalia namna bora ya kutangaza vivutio vya utalii vya mikoa hiyo , kutoa elimu kwa umma kuhusu uhifadhi na utalii pamoja na kujitahidi kutoa misaada kwa jamii (Community Social Responsilbility-CSR)kwa kadri fedha za ziada zinavyopatikana.
Ameahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali za migogoro ya mipaka, migogoro kati ya wanyamapori wakali na waharibifu na binadamu katika maeneo ya hifadhi ya Mikoa hiyo na kuendelea kushirikiana kwa karibu katika utendaji kazi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wabunge wa Mikoa ya Rukwa na Katavi pamoja na baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS)




Post a Comment