Rais wa Hungary amejiuzulu akiwa mubashara kwenye TV kutokana na uamuzi wa kutoa msamaha kwa mtu aliyefungwa kwa kukutwa na hatia ya kuficha taarifa muhimu kwenye kesi ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto.
Wiki iliyopita, taarifa zilitolewa kuwa Rais Katalin Novak alitoa msamaha kwa mtu aliyefungwa gerezani kwa kulazimisha watoto kubadili kauli zao kuhusiana na tuhuma za unyanyasaji wa kingono dhidi ya mkurugenzi wa kituo cha serikali cha kulelea watoto.
Kulikuwa na ongezeko la watu wakitaka Rais huyo ajiuzulu.
Bi Novak aliomba radhi na kusema alifanya “makosa” kwa kutoa msamaha huo.
Judit Varga, Waziri wa zamani wa Sheria, ambaye aliidhinisha msamaha huo, naye amejiuzulu.
Utata huu ambao umesababisha kujiuzulu huku umekuja baada ya majina ya watu 25 waliopewa msamaha na Bi Novak mwezi Aprili mwaka jana, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Papa Francis.
Majina hayo yalitolewa na vyombo vya habari wiki iliyopita.
Upinzani nchini Hungary Pamoja na waandamanaji wamekuwa wakimtaka ajiuzulu, ingawa uamuzi wake wa kufanya hivyo kwenye TV umeonekana wa ghafla na ambao haukutarajiwa.
Bi Novak ni maarufu kwenye chama tawala cha Fidesz, na mwanasiasa haba wa kike kwenye siasa zinazotawaliwa na wanasiasa wanaume.
Mwaka 2022 alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Hungary, nafasi ambayo sio ya kiutendaji.
Mwaka 2023 Bi Katalin Novak alifanya ziara nchini Tanzania.

Post a Comment