Na Mwandishi Wetu,Kigoma
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor H. Seff amekutana na watumishi wa
TARURA Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma ambapo amepokea taarifa mbalimbali za
kiutendaji na kuwataka kuzingatia uadilifu na kutimiza wajibu.
Ameyasema hayo alipokuwa kwenye
kikao na watumishi wa TARURA wilayani humo kwa lengo la kupata mrejesho na
kuangalia kama kuna changamoto ziweze kupatiwa ufumbuzi na watumishi walipata
fursa ya kutoa maoni yao lengo likiwa ni kuboresha utendaji ili kuendelea kutoa
huduma kwa wananchi.
"Nimepata nafasi ya kumsikiliza kila
mmoja wenu na changamoto zilizo ainishwa zitafanyiwa kazi, wito wangu kwenu ni
kuhakikisha kila mtu anatimiza wajibu wake kwa wakati na kwa uadilifu ili
tuweze kufikia malengo kwa kutoa huduma bora ya usafiri na usafirishaji
kwa wananchi", amesema Mhandisi Seff.
Mhandisi Seff anaendelea na ziara ya ukaguzi
wa miradi katika Wilaya ya Buhigwe ambapo pia atakagua ujenzi wa Barabara ya
Kasulu-Kabanga-Kasumo-Muyama- yenye urefu wa km 36 kwa kiwango cha lami ambapo
ujenzi wa km 12.5 unaendelea kwa awamu ya kwanza.
Post a Comment